Micheweni FM

ZEC yatagaza tarehe ya kuanza uandikishaji wapiga kura awamu ya kwanza 2023

19 November 2023, 1:18 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)Jaji George Joseph Kazi akizungumza na wadau wa uchaguzi kuhusu uandikishaji wapiga kura wapya (picha na Mwiaba Kombo)

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(c)cha sheria ya kuanzisha afisi ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar namba 1ya mwaka 2017 na sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka mwaka 2018,imepewa jukumu la kuandaa ,kutayarisha ,kuhifadhi na kuendeleza daftari la kudumu la wapiga kura.

Na Mwiaba Kombo

Jumla ya wapiga kura wapya wapatao laki moja sitini na mbili elfu mia sita na sita 162,606 wanatarajiwa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga ambalo linatarajiwa kuanza tarehe 2 Disember na kumaliza tarehe 15 Januari 2024.

Akitoa taarifa kwa wadau wa uchaguzi katika ukumbi wa Makonyo Chake Chake Pemba Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji  George Joseph Kazi amesema jukumu ambalo linaikabili tume linahitaji kutekelezwa kwa kipindi hiki ,hivo ni vyema kushirikiana katika kufanikisha suala hili.

Aidha amesema uandikishaji huu utawahusu wapiga kura wapya tu ambao kimsingi hawajawahi kuandikishwa katika daftari la  kudumu la wapiga kura ,zoezi ambalo litafanyika kwa muda wa siku tatu 3 kwa kila kituo kilichopangwa na Tume.

Kazi amewaomba wananchi na wadau wote wa uchaguzi wa Zanzibar kudumisha Amani kabla ,wakati na baada ya uchaguzi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa uchaguzi Zanzibar Thabiti Idarous Faina amesema katika uandikishaji huu mpya ,vyama vya siasa vimepewa fursa ya kupeleka mawakala wao katika kila kituo ambacho kitaandikisha wapiga kura wapya .

Faina amewataka wale wote ambao kutokana na sababu moja au nyengine hawakupata fursa ya kuhakiki na wale ambao wametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea na wanavyo vitambulisho vya Mzanzibar mkaazi na ni wakaazi wa maeneo wanayoomba kuandikishwa na hawajawahi kuandikishwa kujitokeza katika zoezi hilo.

Nae mkurugenzi wa kurugenzi ya huduma za sharia kutoka tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)Maulid Ame Mohammed ameeleza kuwa kifungu cha 5 cha sharia ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 kimeanzisha daftari kwa ajili ya uchaguzi ,hivo ni jkumu la tume ya uchaguzi kutayarisha daftari na kuhifadhi daftari hilo makao makuu.

Nao washiriki wa mkutano huo wameihakikishia tume hiyo kushiriki kwa silimia zote kuhakikisha zoezi hili linakwenda kwa salama na amani bila ya kuwepo na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa Amani.

Akifunga mkutano huo ya mmoja kati ya wajumbe wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)Halima Mohammed Said amewataka waaandishi wa habari kuisaidia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)katika zoezi hili la uandikishaji wa wapiga kura wapya katika daftari la kudumu.

Zoezi hili la uandikishaji wapiga kura wapya litaanza rasmi tarehe 2 desember 2023 katika wilaya ya Micheweni na kumaliza tarehe 15 January 2024 katika wilaya ya Mjini.