Micheweni FM

PEGAO, TAMWA watoa neno kuhusu vyeti bandia

18 October 2023, 11:19 am

Mkurugenzi wa PEGAO Hafidh Abdi Said akizunguma na wadau mbali mbali wa haki za binadam juu ya upatikanaji wa vitambulisho pamoja na vyeti (picha na Mwiaba Kombo)

Tatizo la upatikanaji wa vitambulisho pamoja na vyeti bandi (feki) limekuwa ni tatizo sugu ambalo kwa sasa katika visiwa vya Zanzibar ni jambo la kawaida licha ya serikali pamoja na wadau wengine kupiga kelele siku hadi siku kuhusu kupatikana kwa huduma hizo.

Na Mwiaba Kombo

Wakala wa usajili na matukio ya kijamii Zanzibar imekumbushwa kuwatumia waandishi wa habari na wadau wengine wa haki za binaadamu ili kuifikia jamii kwa lengo la kuielimisha na kuepukana na vyeti na vitambulisho feki katika jamii.

Akifungua mkutano  Mkurugenzi wa mradi wa kuihamasisha jamii kudai haki zao za uongozi, siasa na demokrasia ‘SWIL’ kutoka Jumuiaya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia ‘PEGAO’ Hafidh Abdi Said katika ukumbi wa chama cha waandishi wa habari TAMWA Chake Chake Pemba amesema bado jamii inahitaji elimu ya kutosha juu ya uapatikanaji wa vyeti na vitambulisho.

Amesema jamii bado imekuwa na changamoto kubwa sana kuhusu masuala kama haya licha baadhi yao kusema kuwa hakuna changamoto yeyote.

Nae Mratibu wa Chama cha waandishi wa Habari Tanzania Zanziba TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, mesema kuwa lengo la  mradi ni kuona jamii inahamasika ili kupata haki zao stahiki, bila pingamizi zozote na sio kwenye nafasi za uongozi pekee, kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya watu.

Amewataka  waandishi wa habari na wadau wengine kuona kwamba kuna umuhimu mkubwa kwao, kuifikia jamii kuwapa elimu juu ya haki mbali mbali za jamii.

Mapema akiwasilisha changamoto zilizoibuliwa na wahamasishaji jamii, juu ya kudai haki zao za uongozi demokrasia na siasa, mtoa mada Khalfan Amour Mohamed amesema  kuwa, bado jamii inatatizo la uelewa mdogo juu ya haki yao ya vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya mzanzibari mkaazi.

Amesema jamii inatakiwa kutumia ofisi ambazo zinatakiwa kutumiwa katika kupata stahiki zao na badala yake kuacha kutumia watu ambao hawahusiki (vishoka )katika upatikanaji wa haki zao.

Kwa upande wake  Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali mkoa wa kusini Pemba, Mohamed Shamte Omar, amezitaka taasisi husika zinazosajili matukio ya kijamii, kuondosha vikwazo pale inapotokezea changamoto mbali mbali, ili jamii isikate tamaa na ofisi hiyo.

Akitoa ufafanuzi wa masuala ambayo yameulizwa na washiriki wa mkutano huo afisa  kutoka Wakala wa Usajili na Matukio ya Kijamii wilaya ya Chake chake Yussuf Iddi Faki, amesema lawama zinazoelekezwa kwao sio sahihi, kwani wao wamekuwa wakiandika taarifa wanazopewa na mlengwa.

Nao waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali kisiwani Pemba wamesema kuwa, kwasasa ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kusimamia majukumu yake ili suala hili liweze kuondoka na kila mtu kupata haki yake ambayo anastahili kuipata.