Micheweni FM
Micheweni FM
17 September 2026, 1:25 pm

Wananchi wa Wilaya ya Micheweni wamesema wamekuwa sehemu ya mafanikio ya elimu ya watoto wao kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo yao kielimu , wakisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanafanya vizuri na kufikia malengo yao ya kielimu.
Na Masanja Mabula.
Wakizungumza katika mdahalo maalum ulioandaliwa na kituo cha redio Jamii Micheweni chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, huko Shumba ya Mjini wananchi hao wamesema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao skuli , pamoja na kushirikiana na walimu katika kutatua changamoto zinazoweza kuathiri masomo yao.
Nao baadhi ya viongozi walioshiriki mdahalo huo, akiwemo Afisa Elimu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na mwakilishi wa UNESCO, wamewataka wanafunzi kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kukwamisha maendeleo yao kielimu, huku wakisisitiza umuhimu wa kujituma katika masomo na kutumia fursa zinazopatikana.
Akifungua mdahalo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi na ushawishi walionao kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu, hususan kwa watoto na vijana.
Mdahalo huo umeweka msisitizo juu ya umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote wa elimu katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri maendeleo yao kielimu.