Micheweni FM
Micheweni FM
7 October 2026, 7:09 am

tukio la kupotea na kuuwawa kwa mwanafunzi Raian Hemed , aliyekuwa mwanafunzi wa Skuli ya Sekondari Kizimbani Wete.
Na Mwamize Mhamed
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, amefika katika Kijiji cha Kwale Mpona, Shehia ya Finya, Wilaya ya Wete, kuwafariji familia ya Bi. Time Ali Omar na Hemed Amour Hemed kufuatia tukio la kupotea na kuuwawa kwa mwanafunzi Raian Hemed, aliyekuwa mwanafunzi wa Skuli ya Sekondari Kizimbani Wete
Akizungumza na familia hiyo wakati wa ziara ya pole, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa wa Kaskazini Pemba umeumizwa na kusikitishwa na tukio hilo, huku akiiomba familia kuwa na subira, uvumilivu na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Amesema Serikali itaendelea kuwa karibu na familia hiyo katika wakati huu wa majonzi.
Aidha, Mgeni Khatib Yahya amewataka wanafunzi wanaoishi katika kijiji hicho kuendelea na masomo yao kama kawaida huku wakizingatia tahadhari za usalama wanapokwenda na kurejea shuleni. Amesisitiza kuwa Serikali ipo pamoja nao na inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha usalama na ustawi wao.
Kwa upande wao, Juma Hamad Khalid na Khamis Hamad Khalid, wakizungumza kwa niaba ya familia, wameushukuru uongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kufika kuwafariji katika kipindi hiki kigumu, wakisema hatua hiyo imewapa faraja na kuwapa moyo katika kukabiliana na msiba huo.