Micheweni FM

“Rusha Roho kufuata Sheria” RC Hamida

9 October 2026, 1:04 pm

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis akizungumza katika mkutano maalum kati ya Masheha wa Mkoa wa Kusini Unguja na viongozi wa Baraza la Sanaa, Filamu na Sensa Zanzibar Picha na Essau Kalukubila.

Masheha wamepata uelewa kuhusu dhamira ya Serikali kupitia Wizara hiyo katika kulinda mila, silka na tamaduni za Zanzibar  na kusema kuwa mabadiliko ya dunia hayapaswi kuwa sababu ya kuachana na tamaduni zilizokuwepo, ambazo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Zanzibar

Na Essau Kalukubila

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amewataka Masheha katika Mkoa huo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo maelekezo ya Serikali kuhusu upigwaji wa ngoma katika kumbi za starehe na maeneo ya wananchi, ili shughuli hizo zifanyike kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Mhe. Hamida ameyasema hayo Tunguu, wakati akizungumza katika mkutano maalum kati ya Masheha wa Mkoa wa Kusini Unguja na viongozi wa Baraza la Sanaa, Filamu na Sensa Zanzibar, mkutano uliolenga kutoa elimu kuhusu taratibu za utoaji wa vibali kwa shughuli za muziki na sanaa.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis,

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, Bwana Mattar Zahor Mattar, amesema Masheha wamepata uelewa kuhusu dhamira ya Serikali kupitia Wizara hiyo katika kulinda mila, silka na tamaduni za Zanzibar  na kusema kuwa mabadiliko ya dunia hayapaswi kuwa sababu ya kuachana na tamaduni zilizokuwepo, ambazo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Zanzibar.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo, Bwana Mattar Zahor Mattar

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Bwana Juma Choum Juma, amesema zuio la upigwaji wa ngoma kiholela lililotolewa na Serikali mwanzoni mwa mwaka huu bado lipo, hivyo Masheha wanapaswa kuendelea kulisimamia ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Bwana Juma Choum Juma

Wakitoa michango yao katika mkutano huo, baadhi ya Masheha wamesema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni baadhi ya waombaji wa vibali kutofuata masharti yaliyowekwa pamoja na baadhi ya waombaji hutumia vibali walivyopewa kwa shughuli tofauti na zile zilizoainishwa wakati wa kuwasilisha maombi yao.