Micheweni FM

Vijana Watakiwa kuwa wabunifu katika kunasa Fursa za Kiuchumi

6 November 2026, 11:14 am

Picha ya Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Vijana na Uwezeshaji, Zawadi Nassor Amour akipewa maelezo na mmoja wa wajaseriamali wa kusarifu zao la mwani na kuwa mafuta na sabuni Picha na Essau Kalukubila.

Kijana Impact kwa kushirikiana na ActionAid Tanzania katika Ukumbi wa Tibilinzi, Wilaya ya Chake Chake Pemba, lililowakutanisha vijana kutoka wilaya zote nne za Pemba, amesema kuwa wakati umefika kwa vijana kuamka na kutumia ipasavyo fursa

Na Essau Kalukubila.

Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Vijana na Uwezeshaji, Zawadi Nassor Amour, amewataka vijana kuwa wabunifu katika kuzisaka fursa mbalimbali zilizopo ili ziwawezeshe kujikwamua kiuchumi na kufikia maendeleo endelevu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Kijana Impact kwa kushirikiana na ActionAid Tanzania katika Ukumbi wa Tibilinzi, Wilaya ya Chake Chake Pemba, lililowakutanisha vijana kutoka wilaya zote nne za Pemba, amesema kuwa wakati umefika kwa vijana kuamka na kutumia ipasavyo fursa zinazowazunguka ili kutimiza malengo yao.

Sauti ya Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar anayeshughulikia masuala ya Vijana na Uwezeshaji, Zawadi Nassor Amour

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar, Salama Mbarouk Khatib, amesema vijana wanapaswa kutambua wajibu wao katika kutunza mazingira kwa kushiriki kikamilifu shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo upandaji wa miti ya mikoko.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha ushirikiano katika jamii pamoja na kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar, Salama Mbarouk Khatib

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Kijana Impact, Hellen Sisya, amesema lengo la kuwashirikisha vijana katika kongamano hilo ni kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuwahamasisha kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto hizo.

Naye Mratibu wa Vijana kutoka ActionAid Tanzania, Arif Fazel, amewataka vijana kuwa wazi kuhusu vikwazo wanavyokabiliana navyo katika maisha yao ili kupata ushauri na msaada utakaowasaidia kufikia malengo yao.

Sauti ya Msimamizi wa Mradi wa Kijana Impact, Hellen Sisya na Mratibu wa Vijana kutoka ActionAid Tanzania, Arif Fazel

Kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na mazingira huku likiwapa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili.