Micheweni FM
Micheweni FM
4 November 2026, 5:54 pm

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii, Mhe. Masoud Ali Mohammed, amezungumzia umuhimu katika kuleta maendeleo endelevu ya Zanzibar, huku akitoa shukrani kwa Mufti Mkuu na kuiomba Ofisi hiyo kuendelea kuimarisha mahusiano na jamii kwa kushiriki
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii, Mhe. Masoud Ali Mohammed, amesema dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na jamii kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na wadau mbalimbali katika kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi, pamoja na kuimarisha maadili na mshikamano katika jamii.
Amesema hayo alipokutana na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, kwa ajili ya kujitambulisha kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Dkt. Mwinyi.
Amesema kuwa ushirikiano kati ya Serikali na viongozi wa dini ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu ya Zanzibar, huku akitoa shukrani kwa Mufti Mkuu na kuiomba Ofisi hiyo kuendelea kuimarisha mahusiano na jamii kwa kushiriki katika masuala mbalimbali yanayolenga ustawi wa wananchi
Naye Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, amesema Ofisi ya Mufti ina nafasi ya kuwa kiunganishi muhimu kati ya jamii na taasisi mbalimbali, na kwamba ipo tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi, Serikali na taasisi nyingine katika kutekeleza majukumu yake.
Wakati huo huo, Mhe. Masoud Ali Mohammed, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, aliwajulia hali Katibu Mufti Mstaafu, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Bi. Mwaka Mrisho Abdallah, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano na kuwapa pole viongozi hao.