Micheweni FM

DC Micheweni amlilia aliekufa kwakufukiwa na Mawe Mjini Wingwi

19 October 2026, 4:27 pm

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Khatib Juma Mjaja akisikiliza maelezo ya mganga wa zamu wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Dr Rafael Philibet baada ya ajali ya mawe kutokea na kuwafunika wajimbaji wa mawe na kusababisha kifa cha mtu mmoja Picha na Essau Kalukubila.

Kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu wengine wawili katika eneo la Mjini Wingwi, Wilaya ya Micheweni, kufuatia sehemu ya mwamba kukatika na kuwaangukia wafanyakazi waliokuwa wakifanya shughuli za uchimbaji wa mawe.

Na Essau Kalukubila.

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Khatib Juma Mjaja, amewataka wananchi wanaojishughulisha na shughuli za kuvunja mawe kuchukua tahadhari kubwa wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeraha yasiyo ya lazima.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza baada ya kutokea kwa ajali ya mawe iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu wengine wawili katika eneo la Mjini Wingwi, Wilaya ya Micheweni, kufuatia sehemu ya mwamba kukatika na kuwaangukia wafanyakazi waliokuwa wakifanya shughuli za uchimbaji wa mawe.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Khatib Juma Mjaja

Akizungumza baada ya kuwapokea majeruhi hao katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni, Mganga wa Zamu, Dkt. Rafael Philibet, amesema kuwa marehemu alipoteza maisha kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata baada ya kuangukiwa na mawe hayo, huku majeruhi wengine wakipatiwa matibabu na hali zao kuendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya.

Sauti ya Dkt. Rafael Philibet

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Mjini Wingwi, Hussan Makame Hamad, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi wanaofanya shughuli za uchimbaji wa mawe kuhakikisha wanakagua kwa makini hali ya miamba kabla ya kuanza kazi ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea. Baadhi ya majeruhi walieleza kuwa ajali hiyo ilitokana na kipande cha mwamba kukatika ghafla wakati walipokuwa wakiendelea na kazi zao.

Sauti ya Sheha wa Mjini Wingwi, Hussan Makame Hamad na manusura wa ajali hiyo