Taka zarundikwa kwenye makazi ya watu mjini Sengerema
30 January 2024, 2:13 pm
Mji wa Sengerema kwa mda mrefu umekuwa ukionekana kuwa na mrundikano wa uchafu kwenye vizimba vilivyopo mjini ambapo Halmashauri imekuwa ikitumia vibarua kuzizoa na baadhi yao wamekuwa wakitoa kwenye vizimba na kwenda kuzimwaga kwenye makazi ya watu.
Na:Emmanuel Twimanye
Wakazi wa eneo la Bujora Mtaa wa Misheni Kata ya Misheni wameilalamikia Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kwa kumwaga taka karibu na makazi yao hali inayohatarisha usalama wa afya zao hususani katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu.
Wametoa malalamiko hayo wakati wakizungumza na Radio Sengerema katika eneo hilo na kusema kuwa wanashangazwa na kitendo cha serikali inayohamasisha wananchi kujikinga na kipindupindu ili hali yenyewe ndiyo chanzo cha kuchafua mazingira kwa kumwaga taka karibu na makazi yao.
Baadhi ya watoto wameeleza kuwa uwepo wa taka hizo zimesababisha athari kwao ikiwa ni pamoja na kuugua tumbo na kukatwa na chupa pindi wanapopita katika eneo hilo.
Balozi wa eneo hilo Samwel Lubinza Fimbo amekiri kumwaga taka hizo karibu na makazi ya watu na kwamba licha ya kumtaarifu mwenyekiti wa mtaa wa misheni na afisa afya wa kata hiyo juu suala hilo lakini wamelikalia kimya jambo hilo.
Mwenyekiti wa mtaa wa misheni Joseph Protas ameshangazwa na kitendo cha Serikali ya wilaya kumwaga taka karibu na makazi ya watu huku akimuomba afisa mazingira wa Halmashauri ya Sengerema kuondoa taka hizo katika eneo hilo .
Naye afisa Mazingira wa Halmahsuri ya wilaya ya Sengerema Tandi Laiza amewaomba radhi wananachi kwa kitendo hicho na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.