Orkonerei FM
Orkonerei FM
16 February 2026, 2:16 pm
Na Nyangusi Olesang’ida

Picha ya Diwani ya Kata ya Kiutu
Diwani wa Kata ya Kiutu, Malaki Marambo, amewashukuru wananchi kwa kumuamini tena na kuahidi kuimarisha ushirikiano ili kuchochea maendeleo ya kata hiyo. Kipaumbele chake kikubwa ni uboreshaji wa miundombinu, akipambania ujenzi wa barabara ya Tarura ya mita 900 kwa kiwango cha lami ili kurahisisha mawasiliano na maeneo jirani.
Marambo amezungumza hayo mapema Asubuhi kwenye kipindi cha Amsha Amsha ambapo amesema Katika sekta ya elimu, ujenzi wa madarasa manne unaelekea kukamilika huku shule ya sekondari ikitarajia kuwa na Kidato cha Nne kwa mara ya kwanza mwaka huu. Aidha, uongozi una mpango wa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita punde tu eneo la ujenzi litakapopatikana, huku maabara za sayansi zikiendelea kukamilishwa.
Kuhusu changamoto ya uharibifu wa mazao, Diwani ameeleza kuwa wanatafuta mbinu mbadala za kuwafukuza wanyama kama kima na nyani wanaoshambulia mashamba ya wananchi. Kwa kuwa sheria haizuhusu kuwaua, jitihada za kitaalamu kupitia Halmashauri zinaendelea ili kulinda mazao ya maparachichi na ndizi ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi hao.