Orkonerei FM

Mwenyekiti Kimelok na mfumo mpya wa michango ya maafa

5 February 2026, 1:22 pm

Picha ya mwenyekiti wa kitongoji cha Kimelok Bwana Hoshimu Saitabau

Na Nyangusi Olesang’ida

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kimelok, wilayani Arumeru, Bwana Hoshim Saitabau, ametangaza mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji wa michango ya maafa, akieleza kuwa sasa wataacha kutumia nguvu na badala yake watajielekeza kwenye elimu na hiari kwa wananchi. Hoshim amebainisha kuwa uamuzi huo umekuja baada ya kuona athari za kutaifisha mali za familia (kama mabati) pale kichwa cha familia kinaposhindwa kuchangia kiasi cha shilingi elfu tano kilichowekwa, jambo ambalo lilionekana kuadhibu familia nzima kwa makosa ya mtu mmoja.

Mwenyekiti huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wetu Nyangusi Olesang’ida kwenye Kurunzi mtaa na ameelezea mafanikio ya mwaka mmoja wa uongozi wake, akitaja upatikanaji wa mashamba ya kilimo ndani ya hifadhi ya msitu wa TFS ambapo takriban kaya 40 zimefaidika. Aidha, amesisitiza kuimarika kwa mwamko wa elimu na afya ya uzazi katika kitongoji hicho, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na uongozi ili kutatua changamoto zilizobaki na kuchochea maendeleo ya kijamii.