Orkonerei FM

Wananchi Wafunga Ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji, Watuhumu Kuhujumu Maendeleo

14 January 2026, 12:00 pm

Na Nyangusi Olesang’ida

Picha ya baadhi ya wananchi wa kijiji cha Olmotonyi wakiwa katika ofisi ya mwenyekiti iliyofungwa

Hali ya sintofahamu imetanda katika kijiji cha Olmotonyi, Kata ya Olmotonyi, Halmashauri ya Arusha DC, baada ya wananchi wenye hasira kufunga ofisi ya Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bwana Severini, wakimtuhumu kuwa kikwazo cha maendeleo.

Wananchi hao, wakizungumza na kipindi cha Kurunzi Mtaani cha Orkonerei FM Radio, wamemnyooshea kidole Mwenyekiti huyo kwa madai ya kuzuia jitihada za ukarabati wa miundombinu ya barabara kijijini hapo. Inadaiwa kuwa kiongozi huyo amekuwa akizuia vifusi na udongo unaoletwa kwa ajili ya kufukia mashimo na kuboresha barabara zinazopitika kwa shida.

Picha ya mwenyekiti wa kijiji cha Olmotonyi

Akifika eneo la tukio kutuliza ghasia hizo, Diwani wa Kata ya Olmotonyi, Bi. Muna Taleb, amewataka wananchi kuwa wapole na kutochukua sheria mkononi. Bi. Muna amethibitisha kuwa tayari amechukua hatua za kiofisi kwa kuwasiliana na Mamlaka husika pamoja na Mtendaji ili kuhakikisha Mwenyekiti huyo anawajibika.

Aliongeza kuwa barabara hiyo ni muhimu na tayari wameiombea kwa TARURA ili iingie kwenye mtandao wa barabara za wilaya, huku akiwatoa hofu vijana na wananchi kuwa hakuna mtu mmoja atakayeweza kuzuia maendeleo ya wengi.

Kwa sasa, ofisi hiyo bado imefungwa huku wananchi wakisubiri hatua madhubuti kutoka kwa uongozi wa ngazi ya juu wa Halmashauri ya Arusha DC.