Orkonerei FM

James Ole Millya aongoza kura za maoni Simanjiro

6 August 2025, 11:36 am

Mbunge wa Bunge la Afrika mashariki Bw.James Ole Millya ambaye ameongoza kwenye kura za maoni jimbo la Simanjiro.(Picha na Evanda Baranaba).

Na Isack Dickson

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro, Ndugu Amos Shimba, ametangaza rasmi matokeo ya kura za maoni kwa nafasi ya Ubunge Jimbo la Simanjiro kupitia mahojiano maalum na Orkonerei FM Radio.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, kura zilizotakiwa ni 16,823, na kura zilizopigwa ni 14,574, huku kura 141 zikiripotiwa kuwa zimeharibika.

Matokeo rasmi ya wagombea ni kama ifuatavyo:

  • James Kinyasi Millya – 6,061 kura
  • Timoth Lengitambi – 3,813 kura
  • Lenana Soipey Lenganasa – 3,375 kura
  • Mwajuma Bakari Ally – 692 kura
  • Mathayo Yaiyai Londross – 285 kura
  • Lekoko Lemburis Ngitiri – 177 kura

Akizungumza na Orkonerei FM baada ya kutangaza matokeo, Ndugu Amos Shimba alisema kuwa hatua inayofuata ni utekelezaji wa mchakato wa vikao vya chama, vinavyohusisha:

  1. Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya
  2. Ngazi ya Mkoa
  3. Makao Makuu ya CCM kupitia Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa

Chama kina utaratibu wake wa ndani wa kuchambua majina haya na kuwasilisha mapendekezo hadi kufikia uteuzi wa mwisho wa mgombea Ubunge. Wanachama wamefanya kazi yao, sasa tusubiri kwa utulivu hadi jina litakapotangazwa rasmi,” alisema Shimba.

Aidha, alitoa wito kwa wanachama na wapenzi wa CCM kuendelea kudumisha mshikamano akisema, “Umoja wetu ndiyo ushindi wetu. Simanjiro tunajipanga kuhakikisha kura nyingi zinakwenda kwa wagombea wa CCM, kuanzia kwa Rais Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi kwa Mbunge na Madiwani.”

Sauti ya Ndg Amos Shimba Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro