Orkonerei FM

Maji bado ni changamoto Lorokare

3 September 2024, 11:06 am

Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha lorokare kata ya Oljoro no.5 wilaya ya Simanjiro wakichota maji katika shimo walilofukua katika korongo ili kupata maji ya kunywa na kufanyia matumizi mengine ya kibinadamu. (Picha Na Evanda Barnaba)

“Kuna changamoto kubwa sana ya maji hapa yani unakuja unafukua korongo hapo kwenye mchanga kisha ndiyo uchote maji bila hivyo hakuna maji”

Wananchi wa kijiji cha Lorokare katika kitongoji cha Songambele wamekuwa wakipitia adha kubwa ya kutokupatikana kwa maji ya kunywa kwa muda mrefu sasa.

Orkonerei fm radio kupitia kipindi cha Nijuze Radio show kimetembelea kitongoji hicho na kushuhudia akinamama na vijana wakichota maji katika mashimo madogo madogo walioyafukua katika mchanga wa korongo ili kupata maji ya kutumia.

Wakizungumza kwa uchungu akinamama na vijana wanasema kuwa wakati mwingi hawahudhurii mikutano wala shughuli zingine za kijamii kwani muda mrefu wanakuwa katika shughuli ya utafutaji maji haswa kipindi cha ukame.

Akizungumza mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Olais Mollel ameiomba serikali na RUWASA wilaya ya Simanjiro kuharakisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wanakijiji hao.