Zaidi ya wasichana milioni 4 hatarini kufanyiwa ukeketaji 2024
8 February 2024, 2:51 pm
Kwa mujibu wa UN Women, zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 duniani kote wamepitia Ukeketaji. Mwaka huu wa 2024, takriban wasichana milioni 4.4 watakuwa katika hatari ya kufanyiwa ukatili huo, hii ikiwa ni wastani wa zaidi ya kesi 12,000 kila siku.
Hata hivyo, utekelezaji wa ukeketaji unaonesha kupungua katika miongo mitatu iliyopita katika nchi 31 zenye data za uwakilishi wa kitaifa kuhusu viwango. Kwa sasa, hali inaonesha karibu msichana 1 kati ya watatu mwenye umri wa miaka 15 hadi 19 amefanyiwa ukeketaji ikilinganishwa na msichana 1 kati ya wawili katika miaka ya 1990.
Takwimu za Demografia ya afya za mwaka 2015 zinaonesha kuwa, asilimia 10 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15-49 wamekeketwa Tanzania wakati takwimu za mwaka 2022 zinaonesha idadi hiyo imepungua kwa asilimia 2 tu ambapo kwa sasa ni asilimia 8 ya wanawake wa umri huo wamekeketwa.
Mtandao huo umesema, wakeketaji wanabuni mbinu mpya na sasa wanawakeketa watoto wachanga.
Kwa mujibu wa wanamtandao huo, ukeketaji wa watoto wachanga, ni ukatili mbaya unaoanza kupoteza haki za watoto wa kike wakiwa na umri mdogo zaidi.
Takwimu za demografia ya afya za mwaka 2022 zimeonyesha kuwa mikoa inayoongoza kwa ukeketaji Tanzania ni Arusha,asilimia 43, Manyara (43), Mara asilimia 28 na Singida 20.
Hata hivyo wadau hao wamesema, kuna mikoa ambayo awali haikuwa na ukeketaji lakini takwimu mpya zinaonyesha kuanzia mwaka 2022 wameanza kufanya ukeketaji.
Siku ya Kupinga ukeketaji hufanyika Februari 6 kila mwaka, ambapo Umoja wa Mataifa, uliitambua rasmi siku hii baada ya kuona athari za ukeketaji kwa watoto wake. Kauli mbiu kwa mwaka ni “Sauti yake Hatima yake; Wekeza kwa manusura kutokomeza Ukeketaji”