Orkonerei FM

TAKUKURU ARUMERU YAKABIDHI MIONGOZO YA MIKAKATI WA KUPAMBANA NA RUSHWA CHINI (TAKUSKA)

20 March 2022, 9:24 am

Mkuu wa taasisi ya kupambana na Rushwa wilaya ya Arumeru mkoa wa arusha akimkabidhi miongozo ya TAKUSKA mkuu wa wilaya ya Arumeru.

Na Nyangusi ole sang’da Arusha.
Taasisi ya kupambana na rushwa TAKUKURU Wilaya ya Arumeru imekabidhi miongozo ya TAKUSKA ambayo ni mikakati ya kupambana na rushwa
Nchini kwa kuwashirikisha vijana wa SKAUTI ,inayolenga kuwapa mafunzo vijana hususani wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kuwa wazalendo, waadilifu,waaminifu na wawajibikaji wangali bado wadogo .

Akimkabidhi Miongozo hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru , Mkuu wa Taasisi ya kupambana na RUSHWA TAKUKURU Wilaya ya Arumeru ,Deo Mtui amesema Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na kuandaa vijana Wazalendo, tarehe 02 Machi 2021 ilizindua TAKUSKA.

Aidha, Mtui amesema Lengo la TAKUKURU kuungana na SKAUTI kutengeneza TAKUSKA ni kuhakikisha vijana nchini wanafundishwa Uzalendo, Uadilifu na Uwajibikaji wakiwa bado wadogo kwa kuzingatia vijana ni Taifa la kesho ambapo Mafunzo hayo yatatolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia vilabu vya kupinga Rushwa katika Shule za Msingi na Sekondari.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango ameipongeza TAKUKURU na SKAUTI kwa mikakati hiyo ya mapambano dhidi ya Rushwa (TAKUSKA) ambapo amezishauri Idara ya Elimu Sekondari na Elimu msingi za Halmashauri mbili za Wilaya hiyo kutafuta ofisi katika majengo ya Serikali kwaajili ya SKAUTI ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wa Kamishna wa SKAUTI Wilaya ya Justice Yona ametoa rai kwa Viongozi,Wakuu wa Idara ya Sekondari na Msingi wa Halmashauri mbili za Wilaya ya Arumeru kuona namna ya kuandaa kikao ili SKAUTI iweze kutoa Elimu kwa Wataalam na kuongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa miongozo hiyo ya TAKUSKA.

Aidha, Hafla hiyo ya kukabidhi TAKUSKA iliyofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru imehudhuriwa na Maafisa Elimu Msingi na Sekondari wa Halmashauri za Meru na Arusha pamoja na Maafisa Taaluma.