Amuua kaka yake kisa shamba la urithi
23 October 2023, 11:55 am
Matukio ya mauaji ya watu wakigombea mali za urithi yameshamiri kwa mikoa ya Kanda ya ziwa hasa yakiwahusisha ndugu wa karibu, ambapo wananchi wamelimba jeshi la polisi kwa kushirikiana na asasi za Kiraia wanalojukumu la kuzidi kutoa elimu zaidi dhiidi ya vitendo hivi.
Na: Joyce Rollingstone.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 80 ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na ndugu yake kwa madai ya kugombea mashamba ya urithi katika kijiji cha Ilunda kata ya Ngoma wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya ndugu na wakazi wa kijiji hicho wamesikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali kumchukulia hatua kali mtu aliyehusika na mauaji hayo ya kinyama .
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Ilunda Theleza Mbinzagula Bujingwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja jina la mwanaume aliyeuawa kuwa ni Elias Mulanda mkazi wa kijiji cha Ilunda, huku akiwaomba wananchi pindi wanapokuwa na migogoro wafike kwa viongozi ama wakae kifamilia ili kusuluhisha badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Naye afisa mtendaji wa kijiji cha Ilunda amesema kuwa tayari wamemkamata mshukiwa anayedaiwa kuhusika na mauaji hayo anayefahamika kwa jina la Alphonce Mulanda kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo Jeshi la polisi wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali teule ya wilaya ya Sengerema kwa ajili ya uchunguzi, huku mkaguzi wa Polisi L. J Komba akiwaasa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi .