Walioripoti kuanza Kidato cha Kwanza Shule ya Sekondari Terrat, Simanjiro 2024 ni asilimia 46 tu.
12 January 2024, 11:19 pm
Wanafunzi wapatao 105 kati ya 226 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza shule ya sekondari Terrat wilaya ya Simanjiro ndio pekee walioripoti shuleni hadi sasa.
Na Baraka David Ole Maika.
Akizungumza na Orkonerei FM Redio Mkuu wa shule ya sekondari Terrat Mwl Julius Raymond Maplani amesema kuwa Wanafunzi 105 walioripoti shuleni tayari na kwa ujumla Shule ilipangiwa Wanafunzi 226 ambapo wasichana ni 96 na wavulana 127 na kuwasihi wazazi na walezi wahakikishe kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza shuleni hapo wanafika shuleni.
Mwalimu Maplani amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa shule ya sekondari Terrat kupangiwa idadi kubwa ya wanafunzi tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2007, na ongezeko hilo la idadi ya wanafunzi inatokana na jitihada za walimu wa shule za msingi.
Aidha Mkuu huyo wa shule ya sekondari Terrat amebainisha kuwa hali ya miundombinu shuleni hapo inaridhisha hivyo sio chanhamoto kwa kupokea idadi hiyo ya wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Terrat japo kwa upande wa mabweni watatoa kipaumbele kwa wale wanafunzi wanaotoka mbali.
Mwalimu Maplani ametoa wito kwa wazazi na walezi wote kuwa waondokane na hofu ya kutomleta mtoto shuleni kwa sababu ya kutokukamilisha mahitaji bali wahakikishe kuwa watoto hao wanaletwa shuleni kwani watapokelewa pamoja na mapungufu yaliyopo.
Mwisho Mkuu huyo wa shule ya sekondari Terrat alisisitiza jamii kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kuotesha miti na kutunza mazingira kwani ndio yanayozungumza hatima ya maisha ya mwanadamu.
Shule ya Sekondari Terrat ni miongoni mwa shule za kata zilizoanzishwa na Serikali wakati wa mpango wa kila Kata kuwa na shule ya sekondari mwaka 2006/2007.