Viongozi wa kimila wilayani Longido, wamuombea Dua Rais Samia
10 December 2023, 11:51 am
Viongozi wa mila wa jamii ya kimasai na viongozi wa dini wamuonbea dua ya heri, mafanikio na ushindi Rais Samia Suluhu Hassan
Na Baraka David Ole Maika.
Viongozi wa mila wa jamii ya kimasai na viongozi wa dini kutoka wilaya ya Longido wameungana pamoja kumuombea dua ya heri, mafanikio na ushindi mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025.
Dua hiyo ya kumuombea Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ilikwenda sambamba na kumbariki mwekezaji wa madini ya rubbi na mkurugenzi wa Sendeu Minning Co.Ltd ndugu Gabriel Sendeu Laizer kwa ushirikiano wake na jamii.
Mwangalizi Mkuu wa makanisa ya Pentekosti (FPCT) wilaya ya Longido Bishop Daniel Kazimoto amewasihi viongozi wa dini kumuombea Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, chama na viongozi wa serikali ili Mungu atende makuu kwa mheshimiwa Rais, serikali yake na chama tawala.
Naye Kiongozi wa Mila Alaiguanani Peter Sangeyon kwa niaba ya viongozi wa mila amesema kuwa madam nyanda za malisho katika wilaya ya Longido ziko salama jamii ya wafugaji hawana sababu ya kutompatia kura zote za ndio Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025
Aidha mwekezaji wa madini ya Rubi na mkurugenzi wa Kampuni ya Sendeu Minning Ltd, ndugu Gabriel Sendeu Laizer amewashukuru viongozi wa mila na viongozi wa dini kwa uamuzi wao wa kujumuika Pamoja kuomba dua ya heri, mafanikio na ushindi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi ujao wa mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Longido mheshimiwa Papaa Nakuta amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotekelezwa ndani ya taifa la Tanzania, mkoa wa Arusha na ndani ya wilaya ya Longido.
Dua hiyo ya kumwombea Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan imefanyika hivi karibuni katika eneo la machimbo ya madini ya rubi Kilimahewa kata ya Mundarara wilayani Longido.