Keifo FM

Marufuku wenye ulemavu kufungiwa ndani

1 October 2026, 12:35 pm

Pichani ni wazazi na watoto wenye ulemavu wakiwa na mwalimu wao Mwanaidi Mshana picha na James Mwakyembe

“Watoto wenye ulemavu wana haki ya kupata elimu, na mambo yote ya msingi yanayo wahusu pamoja na kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii inayo wazunguka”.

Na James Mwakyembe

Wazazi na walezi wilayani kyela wametakiwa kuacha tabia ya kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu kwa lengo la kuwaficha badala yake wawapeleka shule ili kupata elimu yao ya msingi inayotolewa katika kituo cha Elimu Maalumu kilichopo shule ya msingi Kyela.

Kauli hiyo imetolewa na mwalimu wa kituo hicho kilichopo katika shule ya msingi Kyela Mwanaidi Mshana ambaye amesema ipo tabia inayofanywa na baadhi ya wazazi na walezi wilayani kyela kuwafungia watoto wenye ulemavu majumbani wakiamini kuwa hawawezi kupata elimu na kufanya shughuli yoyote inayoweza kuwapatia kipato.

Akizungumza na Keifo Fm Mshana ameeleza kuwa watoto hao wakifundishwa wanafundishika na ni muhimu kuwapatia elimu ili waweze kujimudu wao wenyewe kwa kufanya shughuli za kiuchumi kama kufuga mifugo na kufanya biashara mbalimbali ikiwa ni chanzo cha kujiingizia kipato na kujitegemea.

Sauti ya Sauti Mwalimu Mshana
Picha ya wazazi na watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye kilele cha furaha

Mshana ameongeza kwa kutoa mfano wa mwanafunzi mmoja mwenye ulemavu wa viungo ambaye kupitia elimu aliyoipata kituoani hapo alipata nafasi ya kwenda nchini China kimichezo na kupata pesa ambazo zimemsaidia kujenga nyumba anayoishi yeye na bibi yake ambapo ni manufaa ya kumpeleka shule mtoto huyo.

Sauti ya Sauti Mwalimu Mshana

Kwa upande wao wazazi ndani ya wilaya ya Kyela wao wameendelea kuwashukuru na kuwapongeza walimu na serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na kituo cha elimu kwa watoto wenye wenye ulemavu wilayani kyela.

Sauti ya wazazi wakishukuru

Watoto wenye mahitaji maalumu wana haki ya kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine na ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha watoto hao wanaenda shule na kupata elimu.