Keifo FM
Keifo FM
23 April 2026, 8:20 pm

“Tuko tayari kushirikiana na jamii kutokana na namna inavyotuunga mkono kwenye bidhaa zinazozalishwa na kiwanda chetu cha Covenant Edible Oil”.
Na James Mwakyembe
Baada ya mkuu wa wilaya ya Kyela Josephine Manase kuomba wadau kuchangia wahanga wa mafuriko yaliyoikumba wilaya mwaka huu Mkurugenzi wa kiwanda cha Covenant Edible Oil Babylon Mwakyambile ametoa na kukabidhi msaada wa chakula kwa mkuu wa wilaya ili kuwafariji wahanga.
Msaada huo uliotolewa leo kwa mkuu wa wilaya ya kyela ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ni Mahindi gunia nane na maharage debe tano.
Akikabidhi msaada huo wa chakula uliopokelewa na katibu tawala wilaya,mwakilishi wa Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha mafuta cha Covenant Edible Oil Frank Mwakapala amesema baada ya kupata ombi hilo mkurugenzi wao aliona ni vema kuungana na Serikali ili kuwafariji wahanga kutokana na kadhia waliyoipata.

Akipokea msaada huo wa chakula kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Kyela,katibu tawala Sabrina Hamoud amemshukuru Babylon Mwakyambile kwa kuitikia kwa wakati ombi hilo licha ya kuchelewa kumpa taarifa huku akimuomba kuendelea kuwaunga mkono katika mambo mbalimbali yanayoihusu wilaya pamoja na kutoa tathmini ya kata zilizokumbwa na mafuriko.
Mbali na kutoa msaada huo Mwakyambile amekuwa mstari wa mbele katika kuungana na jamii ya wanakyela katika nyanja mbalimbali.