Keifo FM

Katule: Wazazi ni aibu mtoto kukosa mahitaji muhimu ya shule kisa krismasi

12 December 2023, 17:10

Picha ya Mwenyekiti wa Halmashari ya wilaya ya Kyela Katule Kingamkono. Picha Nsangatii Mwakipesile

Wazazi na walezi wilayani Kyela wametakiwa kuweka akiba kwa ajili ya watoto wao kwenda shule mwezi Januari kwani ni jambo la aibu mtoto kushindwa kwenda shule kwa sababu ya krismasi.

Na Nsangatii Mwakipesile

Kuelekea kuhitimisha mwaka wa 2023 mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Katule Godfrey Kingamkono ameshukuru wananchi wote kwa ushirikiano walioutoa katika shughuli zote za maendeleo ndani ya wilaya ya Kyela.

Ametoa pongezi hizo wakati akitoa neno la kuwatakia heri ya sikukuu ya krismasi wananchi wote ambapo katika salamu zake amemshukuru mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kyela kwa ushirikiano walioonesha hasa katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Kadhalika Katule amempongeza mbunge wa jimbo la Kyela Ali Mlagila Jumbe kwa namna alivyokuwa bega kwa bega na jimbo lake hali aliyoitaja kuwa imerahisisha kazi za maendeleo katika wilaya.

Pia amemshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasani kwa kutoa fedha za kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa halmashauri yake na kuendelea kumwomba Rais kusimama pamoja nao.

Amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa Kyela kuzitumia vizuri sikuuu hizi mbili hasa kwa kuhakikisha wanaweka akiba itakayowawezesha watoto wao kutokwama mwezi Januari kupata mahitaji muhimu ya shule.

Saiti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela Kuwatakia heri ya krimasi na mwaka mpya wananchi wote.