Wataalam wa afya kutoka halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na Kanada watoa huduma za afya Terrat.
21 February 2024, 7:28 pm
Wataalam wa afya kutoka halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa kushirikiana na wataalam wa afya kutoka Kanada kupitia shirika la Africa Afya Initiative – AAI wanatoa huduma mbalimbali za afya katika zahanati ya Terrat, wilayani Simanjiro.
Na Baraka David Ole Maika.
Orkonerei FM Radio imefika katika zahanati ya Terrat na kushuhudia wananchi wake kwa waume, watoto na vijana kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya kijiji cha Terrat waliofika eneo hilo la zahanati kupata huduma.
Akizungumza na Orkonerei FM Radio, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Terrat Dr Tumaini Kamkama, amesema kuwa huduma hiyo ni msaada kwa wakazi wa Terrat na vijiji vya jirani kupata huduma zote za kimsingi za afya.
Baadhi ya wananchi waliofika zahanati ya Terrat kupata huduma Jackson Masawe na Hellena Joshua wamesema kuwa huduma zinazotolewa ni nzuri na utaratibu wa mapokezi hadi kuhudumiwa unafurahisha na inawapunguzia gharama ya kwenda mbali kutafuta huduma.
Naye mkurugenzi wa shirika la Africa Afya Initiative – AAI, Bw Steven Martine amesema kuwa mpango huo wa huduma ya afya unawezeshwa na shirika la Canadian African Community Health Alliance – CACHA, kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wanajamii na katika maeneo ya kutolea huduma za afya ndani ya jamii.