Changamoto za shule ya msingi Kitengule kutatuliwa
13 July 2024, 10:30 am
Na Eliud Henry
Changamoto mbalimbali kwa shule za msingi na sekondari nchini zimekuwa kikwazo cha ufaulu na maendeleo ya watoto hasa linapokuja suala la miundombinu mibovu au chakavu na mabweni kwa wenye mahitaji maalum
Shule ya msingi Kitengule inayohudumia watoto wa kawaida na wenye mahitaji maalum katika kata ya Kihanga wilayani Karagwe mkoani Kagera inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwepo kukosa mlinzi wa shule, bwalo la chakula pamoja na uchakavu wa bweni linalotumiwa na watoto wenye mahitaji maalum.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya Karagwe Julius Kalanga Laiser pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya iliyofika shuleni hapo Julai 11, 2024 kwa lengo la kutembelea na kukagua miundombinu ya shule hiyo, mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Sara Bwire Ndaro amaesema kuwa endapo changamoto hizo zitatatuliwa wataongeza ufaulu na kufanya kazi yao kwa uhuru zaidi.
Akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa niaba ya kamati ya ulinzi na usalama, Mkuu wa Wilaya Julius Laiser ameahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazoikumba shule hiyo kama anavyosikika ambapo pia Katibu Tawala wa wilaya Karagwe Rasuli Eliud Shandala amekiri kupokea kero hizo na kusema kuwa atafanyia kazi maelezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya.