Karagwe FM

CHADEMA Kagera: Kamatakamata ya polisi ni kufunika moto kwa nyasi

14 August 2024, 9:20 am

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kagera mwalimu Gratian Mukoba (wa kwanza kulia) akiwa na viongozi wengine wa mkoa. Picha na Theophilida Felician

Viongozi wa vyma vya upinzani nchini na mashirika ya kutetea haki za binadamu wameendelea kulaani tukio la jeshi la polisi mkoani Mbeya na Tanzania kwa ujumla kuzuia kongamano la baraza la vijana wa CHADEMA BAVICHA wakidai kuwa kitendo hicho ni ubaguzi wa kisiasa

Na Theophilida Felician.

Viongozi wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoa wa Kagera wametoa tamko la kulaani matukio ya kuwakamata na kuwashikilia viongozi kadhaa wa chama hicho taifa.

Viongozi hao ambao ni mwenyekiti wa chama mkoa Gratian A. Mkoba, Danieli Damiani pamoja na wengine wametoa maelezo hayo tarehe 12 Agosti, 2024 mbele ya vyombo vya habari katika ofisi za chama mkoa zilizopo kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba.

Wamewataja baadhi ya viongozi hao kuwa ni pamoja na mwenyekiti wa chama taifa Freeman Mbowe, makamu mwenyekiti bara Tundu Lissu, katibu mkuu John Mnyika, Mwenyekiti wa BAVICHA John Pambalu, Mwenyekiti wa kanda ya Nyasa bw.Joseph Mbilinyi na wengineo.

Wamefafanua kwamba yote hayo yamejitokeza kufuatia sakata la vyombo vya usalama likiwemo Jeshi la Polisi kufanya jitihada mbalimbali kulizima kongamano la wiki ya vijana lililokuwa limeandaliwa na BAVICHA kufanyika jijini Mbeya tarehe 12 Agost 2024.

Aidha wamesema kuwa kitendo cha kuzimwa kwa kongamano hilo hakutoizuia CHADEMA kuendelea na mapambano dhidi ya kuzikabili hujuma zenye nia ya kuididimiza CHADEMA.

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kagera mwalimu Gratian Mukoba

Wakati huo huo viongozi hao wameweka sawa taarifa iliyotolewa Agost 10,2024 na chama cha mapinduzi CCM kikiaminisha umma kuwa katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera amekihama chama na kujiunga na CCM jambo ambalo siyo la kweli bali waliyemtangaza Dunstan Mutagahywa ni aliyewahi kushika wadhifa huo na akajiengua mwenyewe.

Katibu Danieli ameongeza kuwa uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya akiwemo katibu ulifanyika mwezi wa tatu mwaka 2024.

Katibu wa CHADEMA mkoa wa Kagera bw. Daniel Damian