Karagwe FM

Wadau watoa mbinu za kuboresha lishe Bukoba vijijini

5 July 2024, 6:18 pm

Baadhi ya wadau wa lishe katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakishiriki kikao. Picha na Theophilida Felician

Suala la ubora wa lishe na mapambano dhidi ya utapiamlo na udumavu kwa watoto mkoani Kagera limekuwa suala mtambuka kutokana na mkoa huu kuwa na wingi wa vyakula lakini ukiendelea kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu na utapiamlo.

Na Theophilida Felician

Wadau mbalimbali katika halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera wamekutana pamoja kujadili jinsi ya kuongeza bidii katika suala la kupambana na changamoto ya udumavu na utapiamlo kwa wananchi.

Wadau hao kutoka maeneo tofauti wamekutana Julai 3, 2024 katika kikao kazi cha lishe kikilenga zaidi taathmini ya utekelezaji wa mradi wa lishe uliokuwa ukitekelezwa na shirika la PANITA kilichofanyika katika manispaa ya Bukoba ambapo katika majadiliano hayo suala la elimu ya lishe limebainika kuwa bado ni changamoto inayowakabili wananchi walio wengi.

Wamefafanua kuwa kutokana na jamii kuwa na uelewa mdogo juu ya ulaji vyakula mchanganyiko na vyenye virutubishi imesababisha baadhi ya wananchi kutokukubali kubadilika na kuendelea kutumia vyakula kwa mazoea wakitoa mfano wa jamii inavyokula chakula aina ya ndizi kwa wingi bila ya mchangayiko wa chakula kingine.

Joseph Matope ni kaimu afisa elimu awali na msingi wilaya ya Bukoba amesema kuwa Bukoba na Kagera kwa ujumla vyakula vipo vya kutosha lakini matumizi yamekuwa ni hafifu mno.

Sauti ya kaimu afisa elimu awali na msingi wilaya ya Bukoba Joseph Matope

Jambo jingine lililoelezwa kuchochea udumavu ni pamoja na baadhi ya wazazi kutokuwa tayari kupokea maelekezo muhimu kutoka kwa watalaamu wa afya juu ya utekelezaji wa lishe, maelezo ambayo yametolewa naye mwalimu Paschal Ngaiza.

“Tunapolisimamia suala hili la lishe tujitowe ufahamu wazazi hawa wengine ni wakorofi wamekuwa wagumu hata kuchangia chakula cha watoto shuleni, hii lishe imekuwa pasua kichwa kwa hiyo tunatakiwa wote kujikakamua na kujipanga vilivyo kuibadilisha jamii yetu hii” mwalimu Paskal akisisitiza.

Afisa mradi wa PANITA Bw. Lubango Charles. Picha na Theophilida Felician

Hata hivyo kwa upande wao PANITA ambao ni mwavuli wa mashirika ya kijamii yanayoshughulika na masuala ya afya na lishe kwa kushirikiana na Gain pamoja na Sanku wanaotekeleza mradi wa urutubishaji chakula shuleni kupitia afisa mradi Lubango Charles wamezitaja shughuli za miradi ya lishe zilizoteketezwa kwa Bukoba DC ikiwemo ya kukutana na viongozi wa halmashauri na wadau wa lishe, kukutana na viongozi wa kata hasa kata ya Kemondo, kuhamasisha uanzishwaji wa bustani za mbogamboga shuleni, wamezifikia shule tano, wamewajengea uwezo watalaamu wa afya ngazi ya jamii, kuelimisha jamii matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa, usimamizi shirikishi katika utekelezaji wa maazimio ya mradi nanyinezo.

Akihitimisha taarifa Afisa Lubango amesema mradi huo kwa sasa umefika kikomo, hivyo ametoa wito akiwasihi wadau wote kupitia nyadhifa zao kujimudu na kuibeba kwa dhati dhana nzima ya lishe kwa kuifuatilia jamii ili kuona kama yanayoelimishwa yanatekezwa kwa ufanisi.

Sauti ya afisa mradi wa PANITA bw.Lubango Charles
Kaimu afisa lishe wilaya ya Bukoba bw. Donald Kalenzo. Picha na Theophilida Felician

Kaimu afisa lishe wilaya ya Bukoba bw. Donald Kalenzo amesema kuwa lishe bora ni jambo ambalo limekuwa likipambaniwa zaidi katika halmashauri ya Bukoba ili kuhakikisha udumavu na utapiamlo unapungua kwa kiwango kikubwa na jamii ibakie kuwa salama kama yalivyo makusudi ya serikali.

Amewahimiza wadau wote kuungana pamoja kuupiga vita udumavu ili kuwalinda watu wote nakuwa na jamii yenye lishe bora kuanzia wanawake wajawazito na watoto.

Joanitha Jovin ni afisa lishe mkoa wa Kagera akipongeza juhudi za PANITA kwa kazi kubwa waliyoifanya Kagera amewakumbusha wadau kuwa udumavu ni adui ambaye anapaswa kutokomezwa ili kuinua afya ya jamii kwani Kagera ni mkoa wenye neema ya vyakula hivyo haina sababu ya kuwa katika hali ya udumavu kama ilivyo kwa sasa.

Sauti ya afisa lishe mkoa wa Kagera bi Joanitha Jovin akitoa elimu ya lishe