EWURA CCC Kagera yaeleza huduma zao kwa wanafunzi
15 June 2024, 3:17 pm
Kumekuwa na pengo kubwa la elimu kuhusu majukumu ya baadhi ya taasisi na wanufaika wa huduma za taasisi hizo ambapo Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati na maji EWURA CCC mkoa wa Kagera limebuni mkakati wa kusambaza elimu kupitia kwa wanafunzi wa vyuo
Na Theophilida Felician Kagera.
Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati na maji EWURA CCC kwa upande wa Mkoa wa Kagera limetanua wigo wa utoaji elimu kwa jamii ambapo limeanza kuwafikia wanafunzi wa vyuo.
Amezungumza hayo wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi Kabale kilichopo Halmashauri ya Bukoba afisa msaidizi huduma kwa wateja na utawala kutoka baraza hilo bi Anadorice Komba na kuongeza kuwa wameona ni vyema elimu hiyo kuipitisha kwa wanafunzi waliopo kwenye vyuo kwa lengo la kuwasaidia ufahamu wa matumizi ya huduma hizo ambazo ni umeme, gesi mafuta na maji.
“Leo tumefika hapa chuo cha Kabale kwa ajili ya kutoa elimu kuhusiana na EWURA CCC namna inavyofanya kazi katika majukumu yetu hasa haki na wajibu wa mtumiaji na vidokezo muhimu kwa mtumiaji wa nishati ya maji, namna ya kuwasilisha malalamiko na mambo mengine yanayomuhusu mtumiaji kwa ujumla, lengo kubwa la kufika hapa ni kwa sababu vyuo vya ufundi ni moja ya wadau wetu muhimu tuliowaweka katika mpango kazi wetu tumefika vyuo kadhaa kikiwemo chuo cha VETA, KING RUMANYIKA na leo tuko KABALE” ameeleza Afisa Komba.
Amefafanua kuwa zoezi la utoaji elimu kwa vyuo ni mwendelezo kwa nia ya kuwafikia wanafunzi wote waweze kuwa mabarozo wazuri juu ya kuieneza elimu zaidi kwenye jamii inayowazunguka.
Amewapongeza viongozi wa vyuo wakiwemo wa chuo cha Kabale kwa jinsi wanavyowapa ushirikiano wa kutosha wanapokuwa wametembelea vyuo hivyo.
Hata hivyo ameendelea kutoa wito kwa wananchi kulitumia baraza hilo kwa namna mbalimbali hususani kupata elimu, kuwasilisha changamoto zinazowakabili kutokana na huduma hizo kwa malengo ya kupata musaada kulingana na jambo husika.
Eustadi Katunzi ni katibu wa kamati ya watumiaji wa huduma za nishati na maji kutoka baraza hilo akitoa elimu amewasihi wanafunzi kuyazingatia yale yote waliyoelimishwa ili yaweze kuwasaidia katika safari yao ya masomo ukizingatia baadhi yao wanasomea masuala ya umeme na maji.
Katunzi pia amewahimiza wanafunzi hao kuongeza bidii kwenye masomo ili kuwawezesha kupiga hatua zaidi.
Kwa upande wao wanafunzi na mwalimu Frolenjon Fedirik wamepongeza EWURA CCC kwa namna walivyo wafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu na kuishauri kuendelea kuwafikia wananchi hususani wale waishio vijijini kwani mara nyingi wananchi hao suala la elimu kupitia nyanja tofauti tofauti huwa ni adimu kwao.