DC Laiser: Wazazi msipuuze chanjo zinazotolewa na serikali
4 June 2024, 11:51 am
Kutokana na ongezeko la magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza serikali kupitia wizara ya afya na kushirikiana na shirika la afua duniani (WHO) wameendeleza utamaduni wa chanjo mbalimbali kwa ajili ya kuzuia magonjwa na ulemavu kwa watoto
Na Ospicia Didace
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera Julius Laiser, amewataka wananchi kuacha kupuuza huduma mbalimbali za chanjo zinazotolewa na serikali kwa watoto, kwani zimethibitishwa na wataalamu wa afya kuwa ni salama kwa afya za watoto
Amesema hayo Juni 3,2024 wakati akizindua kampeni ya chanjo ya matone ya vitamini A kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi miaka mitano iliyozinduliwa katika kituo cha Afya Kayanga wilayani Karagwe ikielezwa kuwa zoezi hilo litaendelea hadi tarehe 30 Juni, 2024
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Henrietha William ambaye pia ni mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii wilaya ya Karagwe kabla ya uzinduzi amesema kwenye kampeni hii kutakuwa na utoaji wa matone ya vitamini A kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi miezi 59 yaani miaka mitano pamoja na utoaji wa dawa za kutibu minyoo kwa watoto wenye umri wa mwaka mmoja hadi miaka 5 sambamba na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto hao.
Kwa upande wake afisa lishe wilaya ya Karagwe bi Lustica Mgumba, amesema lengo la kufanya kampeni hii ni ili kusaidia watoto kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kuhara ili kuunusuru mkoa wa Kagera kuondokana na udumavu na utapiamlo.
Kampeni ya chanjo hiyo hutolewa mara mbili kwa mwaka yaani mwezi wa sita na wa 12 na kauli mbiu ya kampeni ya chanjo ya matone ya vitamini A, ni “Huduma za mwezi wa afya na lishe ya mtoto ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo ya mtoto, tumfikie kila mtoto mahali popote alipo”