Zenj FM

Mbunge Fuoni awakumbuka wenye mahitaji maalum

20/03/2026, 22:29

Mbunge wa Jimbo la Fuoni, Asha Hussein Saleh,akikabidhi sadaka ya nyama kwa wananchi wenye uhitaji maalum katika jimbo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Fuoni, Asha Hussein Saleh, amegawa nyama ya ng’ombe kwa zaidi ya wananchi 200 ili kuwawezesha kusherehekea Eid el-Fitr kwa furaha. Hatua hiyo imelenga kuwasaidia wenye mahitaji maalum hasa.

Na Mary Julius

Katika kuhakikisha wananchi wenye mahitaji maalum wanasherehekea Sikukuu ya Eid el-Fitr kwa furaha na amani, Mbunge wa Jimbo la Fuoni, Asha Hussein Saleh, ametoa sadaka ya nyama ya ng’ombe kwa zaidi ya wananchi 200 katika jimbo hilo.

Akizungumza mara baada ya zoezi la ugawaji wa sadaka hiyo, Mbunge huyo amesema lengo kuu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kusherehekea sikukuu hiyo bila ya kubaguliwa.

Ameeleza kuwa amechagua kugawa nyama hasa katika kipindi hiki kwa kuwa bei zake hupanda, hali inayowafanya baadhi ya wananchi kushindwa kuimudu.

Aidha, amesisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa mafundisho ya dini yanayohimiza kusaidiana na kuwajali wenye uhitaji, ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika furaha ya sikukuu.

Sauti ya Mbunge wa Jimbo la Fuoni, Asha Hussein Saleh.

Kwa upande wao, wanufaika wa msaada huo wamemshukuru  Mbunge huyo kwa kuwakumbuka na kuwajali, wakisema msaada huo umewapa faraja kubwa na kuwawezesha kusherehekea Eid kwa furaha.

 Aidha wamewahimiza watu wengine wenye uwezo kuiga mfano huo kwa kuwasaidia wahitaji ili jamii nzima iweze kusherehekea kwa mshikamano na upendo.

Sauti Wananchi Fuoni.