Zenj FM
Zenj FM
25 February 2026, 3:25 pm

Na Mary Julius.
Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Seifee Hospital Zanzibar Limited, Samuel Estomih, amesema lengo la kuandaa mashindano ya Ramadhan Football League ni kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za afya Zanzibar.
Amesema hayo wakati wa mchezo wa fainali wa mashindano hayo uliofanyika katika viwanja vya Maisara , ambapo timu ya Al Rahma Hospital iliibuka mshindi kwa kuifunga timu ya Zanzibar Health Service Fund (ZHSF) kwa mabao 2–0.
Estomih ameeleza kuwa michuano hiyo ni muhimu katika kudumisha amani, kuimarisha maelewano na kujenga mahusiano bora kati ya taasisi za afya zinazohudumia wananchi wa Zanzibar.
Akizungumzia ushiriki wa Zanzibar Electricity Corporation (ZECO), amesema ni taasisi muhimu katika sekta ya afya kwani bila huduma ya umeme, huduma nyingi za afya haziwezi kutolewa ipasavyo.
Aidha, ameahidi kuwa mashindano hayo yataendelea kufanyika kila mwaka na waandaaji watazifanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza ili kuhakikisha mashindano yajayo yanakuwa bora zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Seifee Hospital Zanzibar Limited, Dkt. Murtaza Haider, amesema mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya afya katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ameongeza kuwa dini ya Kiislamu inasisitiza umuhimu wa afya na kuishi kwa upendo na majirani kama njia ya kujenga jamii imara.
Naye nahodha wa Al Rahma Hospital, Ali Mohamedi Ali, amesema mashindano hayo ni mazuri na yanapaswa kuendelezwa kila mwaka ili kukuza vipaji na mshikamano.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu ya ZHSF, Abdillahi, amesema licha ya kushindwa kutwaa ubingwa, wanawapongeza waandaaji kwa maandalizi mazuri ya mashindano.
Ameishauri kamati ya maandalizi kuimarisha utaratibu wa ukaguzi wa vitambulisho vya wachezaji ili kuzuia ushiriki wa wachezaji wasio halali na kuhakikisha ushindani wa haki.
Mashindano hayo ya siku tano yameandaliwa na Seifee Hospital Zanzibar Limited na yalizikutanisha timu nane ambazo ni: Seifee Hospital, Wizara ya Afya, ZHSF, Ampola Hospital, Al Rahma Hospital, ZECO, Tawakkal Hospital na Lumumba Hospital.
Mshindi wa kwanza amekabidhiwa medali pamoja na kitita cha shilingi milioni moja, huku mshindi wa pili akipata medali na shilingi laki tano.