Zenj FM

Soraga afunguka, jinsi mfumo wa anuani utakavyorahisisha biashara na huduma Zanzibar

13 February 2026, 9:07 pm

Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar,Mudrik Ramadhan Soraga, akikabidhi mfano wa ufunguo wa gari kwa ajili ya usafirishaji wa vifurushi mbalimbali.

Na Berema Nassor.

Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar,Mudrik Ramadhan Soraga, amesema uanzishwaji na utekelezaji wa mfumo wa anuani za makaazi ni hatua ya kimkakati inayolenga kurahisisha utambuzi wa makaazi, biashara na taasisi, sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma za posta, usalama wa dharura, ukusanyaji wa mapato na mipango ya maendeleo.

Akizungumza na viongozi mbalimbali katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Shirika la Posta Tanzania upande wa Zanzibar, Waziri huyo amesema shirika hilo limekuwa mdau muhimu katika utekelezaji wa mfumo huo kupitia uzoefu wake wa muda mrefu katika usambazaji wa huduma za posta na vifurushi.

Sauti ya Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar,Mudrik Ramadhan Soraga

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Anuani za Makaazi nchini Tanzania kutoka wizara hiyo, Edith Turuka, amesema mfumo wa anuani za makaazi ni nyenzo muhimu katika safari ya kuelekea uchumi wa kidijitali na hata uchumi wa buluu kwa upande wa Zanzibar.

Sauti ya Mkurugenzi Msaidizi wa Anuani za Makaazi nchini Tanzania kutoka wizara hiyo, Edith Turuka.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mbarouk Khamis, amesema utekelezaji wa mfumo huo unaendelea vizuri na umeleta mafanikio makubwa kutokana na mashirikiano kati ya serikali, Shirika la Posta na mamlaka za serikali za mitaa, hatua iliyosaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mbarouk Khamis.

Katika hafla hiyo, Shirika la Posta Zanzibar limekabidhiwa vitendea kazi vikiwemo gari, bajaji na vishkwambi, kwa lengo la kurahisisha na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mfumo wa anuani za makaazi.