Zenj FM
Zenj FM
9 January 2026, 12:02 am

Na Mary Julius.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uwekezaji wa Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM–IMS) iliyopo Buyu, Wilaya ya Mjini Magharibi B, Zanzibar, utakuwa chachu ya uchumi jumuishi na kuongeza tija pamoja na kipato cha kizazi cha sasa na kijacho.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwekeza katika elimu ya juu, utafiti na maendeleo ya sayansi kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya Taasisi ya Sayansi za Bahari hayapaswi kubaki ndani ya chuo pekee, bali yanapaswa kugusa moja kwa moja jamii inayokizunguka.
Hivyo, ameagiza Taasisi hiyo kuanzisha na kuimarisha mafunzo ya muda mfupi kwa vitendo kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi, hususan wakazi wa Buyu na maeneo ya jirani.
Akizungumza na wanafunzi wa taasisi hiyo, Rais Samia amewahimiza kutumia fursa za elimu na miundombinu ya kisasa kufanya tafiti bunifu zitakazolinda na kuendeleza rasilimali za bahari, ambazo ni mhimili muhimu wa uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kukamilika kwa jengo hilo ni matokeo ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika elimu ya sayansi na tafiti.
Amesema mradi wa HEET umeiwezesha IMS kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi, kuimarisha tafiti za uchumi wa buluu na kuanzisha programu mpya sita za kitaaluma.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema Uzinduzi wa Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu unaashiria hatua mpya ya maendeleo ya elimu ya bahari nchini na matarajio ya Taasisi hiyo kuwa kitovu muhimu cha sayansi ya bahari kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.