Zenj FM
Zenj FM
13 August 2025, 4:29 pm

Na Mary Julius.
Waandishi wa habari wametakiwa kushirikiana kwa karibu na wizara ya Afya Zanzibar kitengo cha chanjo ili kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo, kwa lengo la kupunguza upotoshaji na dhana potofu zinazohusu chanjo.
Afisa kutoka Kitengo cha Chanjo Zanzibar, Ruzuna Abdulrahim Mohamed, ameyasema hayo katika semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, iliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Zanzibar.
Ruzuna amesema waandishi wa habari ni mabalozi muhimu katika kuhamasisha jamii kuhusu huduma za chanjo na faida zake, kwa kuwa jamii inawategemea kupata taarifa sahihi na zenye kuaminika.
Aidha, amesema chanjo zinazotolewa Zanzibar ni salama na zimeshawahakikishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na kuidhinishwa na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA).
Kwa upande wao, wauguzi waliohudhuria semina hiyo wamewasihi waandishi wa habari kuandaa vipindi maalum vinavyolenga moja kwa moja jamii kuhusu umuhimu wa chanjo, na kuhakikisha watoto kuanzia siku ya kuzaliwa hadi miaka mitano wanapokea na kukamilisha dozi zote kwa wakati.
Aidha wameiomba jamii kuwahamasisha na kuwaruhusu mabinti zao wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kupokea chanjo ya shingo ya kizazi (HPV), ambayo ni kinga madhubuti dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Nao Washiriki wa semina hiyo wameahidi kutekeleza maelekezo hayo kwa kuandaa vipindi na makala zitakazosaidia kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo, ili kujenga taifa lenye afya bora na lisilo na magonjwa.