Zenj FM
Zenj FM
30 May 2025, 6:09 pm

Kusini Unguja
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja Mussa Haji Mussa amewaasa wananchi wa Wilaya ya Kusini kudumisha usafi katika maeneo yao ili kubadilisha haiba ya miji ya Wilaya hiyo.
Ameyasema hayo wakati wa zoezi la usafi katika nyumba za madaktari Kitogani ikiwa ni uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira ndani ya Wilaya ya kusini.
Amesema kwa sasa Halmashauri imekuja na mkakati wa kung’arisha maeneo yote ya Wilaya ya Kusini, hivyo amewaomba Masheha wa Wilaya hiyo kushirikiana na Halmashauri katika kuhakikisha miji inakuwa safi na kutimiza ndoto ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa safi na kuwa kivutio kwa watalii.
Aidha ameeleza kuwa Halmashauri imeandaa operesheni maalum kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mifugo yote inayozurura inadhibitiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Mustafa Mohammed Haji amesema wameamua kufanya usafi katika eneo ikiwa pia ni matayarisho ya kupokea Mwenge wa Uhuru hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mbio za Mwenge wa Uhuru.
Nae Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya Kitogani Dkt. Bakari Mohammed Faki ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kusini kwa kuamua kuwaunga mkono kwa kufanya usafi katika eneo hilo.