Zenj FM
Zenj FM
22 May 2025, 4:05 pm

Na Is-haka Mohammed Pemba
Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar sasa inafikia miaka 26 tokea kuanzishwa kwake ambayo ni Sheria nambari 7 ya mwaka 1997, pamoja na majumuisho na marekebisho yake na. 1 ya mwaka 2010.
Sheria hii, imetungwa mahsusi kusimamia na kuangalia mwenendo wa vyombo vya habari Zanzibar hasa vile vya kielekroniki ikiwamo radio, televisheni na vile vyombo vinavyorusha maudhui yake kwa njia ya mtandao.
Sheria hii ambayo ina jumla ya vifungu 30, vikiwa mgawanyo wa sehemu sita kuu, ndani yake vipo vifungu sio rafiki, kuelekea uhuru kamili wa habari hapa visiwani Zanzibar.
Itakumbukwa kuwa Disemba 10, ya 1948 Shirika la umoja wa Mataifa katika Mkutano wake uliweza kupitisha azimia la haki za binadamu ambapo katika azimio hilo lilizungumzia juu ya uhuruwa habari na kujieleza ikiwa ni haki muhimu kwa binadamu kuzifikia kwa urahisi haki zake za msingi.
Vifungu ambayo ni hatari kwa uhuru wa habari Zanzibar Vipo vifungu kadhaa, ambavyo vinaonekana kuwa ni tishio kwa uhuru wa habari, lakini kifungu kimoja wapo, kinachotishia zaidi na kuweza kutia doa uhuru wa habari hapa Zanzibar ni kile cha 13 (5).
‘’Mtu yeyote asiyeridhika na uamuzi wa Tume kutoa au kataka maombi, anaweza kukata rufaa kwa Waziri kwa namna ya njia itakavyoelezwa na kanuni,’’ kinaeleza kifungu hicho.
Hapa, muombaji leseni (kwa mfano mwandishi wa habari), anapokataliwa kupewa leseni na Katibu Mtendaji wa Tume, akate rufaa kwa waziri, ambae ndie aliyemteua Katibu huyo.
Kifungu hiki bado kinambakisha muombaji wa leseni kubaki katika mamlaka ile ile ya Serikali inayoongozwa na Waziri jambo ambalo linaweza kutia shaka kwa muombaji wa leseni kwani Waziri anayehusika anaweza hata kurudi kwa Katibu Mtendaji kutaka ushauri wa hatua aliyoichukua kwa mlalamikaji.
Wakati Salim Said Salim, mwandishi Mkongwe na mjumbe wa Kamati ya Wataalamu wa Habari Zanzibar (ZAMECO) anasema pamoja na sheria ya habari kuwa ni ya muda mrafu lakini ina mapungufu mengi ndani yake yanayochangia waandishi wa habari kutofanya kazi zao kwa uweledi kutokana na kubanwa baadhi ya vifungu katika sheria.
Baadhi ya waandishi wa habari Pemba wakiwa katika mafunzo juu sheria za habari
yaliyoandaliwa na Tamwa-Zanzibar.
Juma Mussa Juma ni Mwandishi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) anasema, kama Tume imekataa kutoa leseni, kifungu kingeelekeza vyenginevyo, kwa mfano anayenyimwa leseni kama hakuridhika ende mahakamani.
Lakini Kifungu kingine ambacho kinaonekana kuwa na maneno yenye ukiukaji wa uhuru wa habari ni kifungu na. 27 (1), ambapo Waziri husika au mwingine aliyeidhinishwa, anaweza kutoa amri kumtaka mpewa leseni (mmiliki wa chombo cha habari), atangaze jambo lolote ambalo kwa maoni ya Waziri, lina maslahi kwa umma au usalama wa taifa.
Wadau wa habari wanasema kuwa, kifungu hicho kipo kishari shari, maana kimempa uwezo mkubwa Waziri, kumlazimisha mpewa leseni kutangaza jambo ambalo anaona tu ni kwa maslahi ya umma au usalama wa taifa.
Mdhamini wa Baraza la Habari Tanzania ‘MCT’ Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema neno kwa maslahi ya umma, sheria hiyo haijalitafsiri, hivyo waziri anaweza kutumia mwanya huo kutangaza jambo ovu.
Mwandishi wa Kituo cha Radio Jamii Micheweni Hadia Faki Ali anasema hilo linajenga hofu kuanzia kwa wamiliki wa vyombo vya habari na mwandishi mmoja moja.
Mwanasheria wa kujitegemea kutoa kisiwani Pemba Khalfan Amour Moh`d amesema kuwa Sheria hii ya Tume ya Utangazaji katika kifungu nambari 27(1) kinaonyesha wazi kuwa bado uhuru wa habari haujapata stahiki zake hapa Visiwani.
“Kama sheria ni haki ya kikatiba, ni vyema isiwe na maneno au amelezo yanayoashiria kumpa mtu mmoja uwezo, kama vile anajiamulia kufanya mambo yake binafsi” amesema Khalfan Amour Moh`d
Alisema ni vyema wanasheria, wanahabari na wadau wengine wakaungana kuona vifungu vya sheria kama hizi zinazopingana na katiba zinaondoshwa kabisa.

Zaina Abdalla Mzee ni Afisa Programmu katika Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA) anasema waandishi wa habari Zanzibar wenyewe wachukue juhudi za kufanya uchechemuzi wa kufanyiwa marekebisho au vile vinavyostahili kufutwa vifutwe kwani wao ndio wahanga wa yote pamoja na wananchi.
WANANCHI
Juma Ali Juma wa Mgogoni Chake Chake Pemba anasema waandishi wasipokuwa huru, hata wananchi wanaweza kukosa uhuru na kushindwa hata kutoa maamuzi yenye maslahi yao na taifa kwa ujumala.
Fatma Bakar Ali wa Mbuzini amesema kuna kama ufinywa wa vyombo vya habari kama televisheni na radio kutokufanya kazi zao kwa kujiamini akieleza pengine ni vile kuwa wamepanwa na
serikali.
Hidaya Mjaka Ali wa Vitongoji ambaye ni mwenye ulemavu wa viungo, anasema, wanavitarajia mno vyombo vya habari, kuibua changamoto za jamii, na hilo litawezekana ikiwa wako huru.
Hata hivyo Sheha wa shehia ya Wara Mchangamdogo, Asaa Makame Said, anasema vyombo vya habari, havipaswi kuwekewa sheria zenye utata, kwani watashindwa kutekeleza kazi zao vyema.
NINI ATHARI YAKE?
Moja wadau wanasema, ni kuwafanya waandishi wa habari kufanyakazi kwa woga na nidhamu iliyopindukia mipaka, huku ikieleweka kuwa, wao kazi yao ni kuitekeleza Katiba.
Mwandishi Malik Shahran wa ZCTV anasema, suala la habari ni haki ya binadamu, si vyema kuwepo kwa sheria inayoonesha nguvu za mtu mmoja kufanya uamuzi.
’Maneno kama Waziri akiweza, atakavyoona inafaa au kwa maoni yake, yanapekelea wengine kukosa hamu ya kuingia kwenye sekta ya habari,’’ anasema Malik Shahran.
Mwandishi wa Mwanahalisi mtandaoni Jabir Idrissa, anasema athari kubwa ni wawekezaji sekta ya habari, kukosa hamu ya uwekezaji, na kundi kubwa kukosa ajira.
Suleiman Said Ali wa Tv ya Mtandaoni ya Jicho Letu iliyopo Pemba, anasema kufuatia sheria hii kandamizi ya Tume ya Utangazaji wakati mwengne waandishi wanakosa kufichua maovu wakihofia kuandamwa.
NINI KIFANYIKE?
Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) Ali Mbarouk Omar, anasema waandishi wa habari na wadau wa habari wanahitajika kuendelea kufanya uchechemuzi wa upatikanaji wa sheria mpya na rafiki ya habari Zanzibar isiyo na vifungu kandamizi, ili sheria mpya ipatikane na waandishi wa habari wafanye kazi zao kama ilivyo, kwa makundi mengine.
Meneja wa Redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, anasema waandishi na wadau wa habari, waungane kushinikiza uswada wa Sheria ya Habari Zanzibar ulipofikia, upelekwe hatua nyingine.Nae Mwandishi wa Radio Jamii Mkoani, Khadija Rashid Nassor, anasema kila mmoja akitekeleza wajibu wake, sheria hiyo kandamizi itaondoka.
Rehema Ramadhani Said wa Kituo cha Radio Jamii Micheweni amesema sasa muda umefika kwa serikali kuthamini machozi ya waandishi wa habari na wadau wao kwa kuifanyia marekebisha au kuunda sheria mpya za masuala ya habari ambazo zitakuwa rafiki kwao.
Hakika huu ni wakati wa kuwapo kwa sheria mpya zinazohusu masuala ya habari hapa Zanzibar, inafahamika kuwa kuna baadhi ya matamko yaliyowahi kutolewa na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita juu ya Mpango wa Serikali wa kuzifanyia marekebisho sheria hizo, lakini kwa kweli kauli hizo sasa imekuwa ni mno.