Zenj FM
Zenj FM
7 May 2025, 4:53 pm

Na Mary Julius.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema serikali ya awamu ya nane ya rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk Hussein Ali Mwinyi katika kipindi cha miaka 4 imewekeza zaidi ya bilioni 380 ili kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa wananchi zanzibar.
Akizungumza katika jukwaa maalum la majadiliano ya masuala ya kuboresha huduma afya kwa vituo vya afya vya wilaya kwa kushirikiana na Pharmacces amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kufanya mambo sita katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora.
Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka Pharm Access Dkt Faiza Abasi amesema PharmAccess imeandaa jukwaa la siku nzima kujadili na kutathmini ubora wa huduma za afya, ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa viwango vizuri.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua kubwa kwa kuwekeza katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali 10 za wilaya, changamoto kubwa inayobakia ni kuhakikisha hospitali hizo zinatoa huduma bora.
Aidha Amesema lengo la PharmAccess ni kuona hospitali hizo mpya zinakuwa mifano ya utoaji wa huduma bora, salama na zenye viwango vya kitaalamu kwa wananchi wote.
Mkurugenzi wa Self-Care Tanzania Dk Peter Rishas ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya kote Zanzibar.
Aidha, ametoa wito kwa watoa huduma za afya kufuata miongozo ya afya pamoja na kutoa huduma bora za afya ili kulinda maisha ya wananchi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango vya kitaalamu vinavyotakiwa.
Wakichangia mada katika jukwaa hilo baadhi ya wadau wa afya wamesema suala la kutoa huduma bora za afya zinawahusu watu wote wanao fanya kazi katika hospitali.
Wadau mbali mbali kutoka Sekta binafsi pamoja na Watumishi wa Wizara ya Afya wameshiriki katika jukwaa maalum la majadiliano ya masuala ya afya na huduma bora katika siku ya tatu ya Wiki ya Afya Zanzibar katika Ukumbu wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.