Karagwe FM

EWURA CCC Kagera yawataka wananchi kuwasilisha malalamiko

24 September 2024, 7:59 pm

Afisa msaidizi huduma kwa wateja na utawala wa baraza la watumiaji wa huduma za nishati na maji EWURA CCC bi Anadorice Komba. Picha na Theophilida Felician

Watumiaji wa huduma za nishati na maji mkoani Kagera wameendelea kunufaika na elimu ya namna ya kuwasilisha malalamiko yao kwenye baraza la ushauri la watumiaji wa huduma hizo EWURA CCC

Na Theophilida Felician

Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za maji na nishati EWURA CCC mkoa Kagera limetoa wito kwa wananchi likiwahimiza kujitokeza katika ofisi za baraza hilo ili kupata huduma kadhaa hususani  elimu  pamoja na kuwasilisha changamoto  dhidi ya huduma za maji na nishati.

Ameyasema hayo Afisa msaidizi huduma kwa wateja na utawala  baraza hilo Anadorice Komba  wakati akitoa elimu kwa wananchi wa kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba na kusema kuwa wananchi iwapo watakuwa na mwitikio mzuri  wa kuifikia ofisi hiyo watanufaika zaidi ikiwemo kupata taarifa sahihi na miongozo katika kuwasilisha  malalamiko.

Amezitaja changamoto zinazowasilishwa na wananchi kwa EWURA CCC kuwa ni pamoja  na wengi wao kufuatilia taarifa zao kwa watoa huduma  bila mafanikio  kutokana na mizunguko ambayo hukutana nayo kutoka kwa wahusika hivyo baraza hilo huchukuwa jukumu  la kuwasadia wananchi  kufuatilia kwa ukaribu kwa malengo ya kupata haki zao.

Afisa msaidizi huduma kwa wateja na utawala bi Anadorice Komba

Hata hivyo ameongeza kuwa wakiwa Rwamishenye wananchi pia wamelalamika na kutoa  maoni pamoja na ushauri kwa mamlaka husika za maji na nishati.

Moja ya malalamiko hayo ni  Ankara kubwa za maji, kukatiwa huduma za maji bila taarifa, pamoja na tozo ya kodi ya majengo kupitia luku ya umeme.

Mwananchi wa Rwamishenye Bukoba bw. Jaziru Yassin akiwasilisha kero yake. Picha na Theophilida Felician

Miongoni mwa wananchi hao yumo Jaziru Yassin ambaye  ametoa ufafanuzi kuhusu kodi ya majengo kupitia luku ya umeme.

Mwananchi wa Rwamishenye Bukoba bw. Jaziru Yassin

Anadorice amewahakikishia wananchi  kuchukuwa malalamiko yao kwa watoa huduma ili yaweze kufanyiwa kazi.