Karagwe FM

Ukatili majumbani wachangia mimba za utotoni Karagwe

10 February 2026, 4:10 pm

Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Karagwe (aliyesimama) bi Owokusima Kaihula. Picha na Jovinus Ezekiel

“Tunaposema unyanyasaji wa kinsia tuna maana ya Matendo au matukio anayoweza kufanyiwa mtu yeyote kwa makusudi kwa lengo la kumuumiza”

Na Shabani Ngarama, Karagwe

Jamii wilayani Karagwe imetakiwa kuachana na migogoro ya kifamilia ili kupunguza wimbi la watoto wa kike wanaopata ujauzito kabla ya wakati baada ya kukimbia majumbani kwenda kutafuta mahali salama pa kuishi.

Wito huo umetolewa na afisa ustawi wa jamii wilaya ya Karagwe na mkuu wa idara hiyo bi Owokusima Kaihula wakati akiongea katika mjadala wa wazi ulioendeshwa na kituo cha Radio Karagwe katika soko la Kakiro kijiji cha Ruzinga kata ya Chanika wilayani Karagwe kwa ufadhili wa shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO hivi karibuni

Amesema kuwa baadhi ya wanawake huvumilia ukatili wanaofanyiwa na waume zao majumbani lakini baadhi ya watoto wa kike wanaofanyiwa ukatili wa kipigo majumbani hukimbilia mtaani ambako hukumbana na wanaume wanaowalaghai na kuwapa ujauzito

Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Karagwe bi Owokusima Kaihula
Privatus Methodius, Picha na Jovinus Ezekiel

Kwa upande wao vijana walioshiriki mjadala huo akiwemo Privatus Methodius mkazi wa kijiji cha Rwambaizi kata ya Kanoni amesema kuwa kichocheo kikubwa cha mimba za utotoni ni tamaa kwa watoto wa kike hasa waliokosa malezi na matunzo ya wazazi wao. Hata hivyo kijana wa kike bi Rehema Mutafungwa mkazi wa Omugakorongo kata ya Kayanga amesema kuwa baadhi ya watoto wa kike hupata mimba za utotoni kutokana na kukosa elimu ya afya ya uzazi kutoka kwa wazazi wanaoendekeza mila zilizopitwa na wakati kwamba mtoto wa kike hapaswi kujua lolote kuhusu uzazi

Rehema Mutafungwa na Privatus Methodius
Rehema Mutafungwa (aliyesimama). Picha na Jovinus Ezekie
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto wilaya ya Karagwe F3035 Staff Sajent Kengela Mayunga (aliyesimama) Picha na Jovinus Ezekiel

Mkuu wa dawati la jinsia na watoto wilaya ya Karagwe F3035 Staff Sajent Kengela ameitaka jamii kuendelea kuelimisha jamii juu ya ulinzi wa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kuacha kuozesha watoto chini ya umri wa miaka 18.

Hata hivyo amesema kuwa baadhi ya kesi wanazozipokea katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Karagwe hutokana na migogoro ya kifamilia ambayo huchangia watoto wa kike kupata madhara ya ujauzito kwa kukosa uangalizi wa wazazi

Mkuu wa dawati la jinsia na watoto wilaya ya Karagwe F3035 Staff Sajent Kengela Mayunga