Karagwe FM
Karagwe FM
6 October 2025, 11:26 am

Malezi kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne ni jukumu la wazazi na walezi sambamba na jamii inayowazunguka wakizingatia kulinda mila na desturi
Na Ospicia Didace, Karagwe
Wazazi na walezi wilayani Karagwe wameaswa kuwatunza watoto wao hata baada ya kuhitimu ngazi mbalimbali za elimu ili kuwawezesha kufikia malengo yao.
Wito huo umetolewa na mgeni rasmi Bw. Longino Wilbard mwanzilishi wa shule hiyo na mgombea udiwani kata ya Chanika kwa tiketi ya chama cha mapinduzi CCM wakati akizungumza katika mahafali ya kwanza ya shule ya sekondari Runyaga iliyohudhuriwa na wazazi, wakuu wa shule na walimu wa shule mbalimbali za jirani, wanafunzi, viongozi wa kijiji, pamoja na wadau mbalimbali wa elimu huku wahitimu wakiaswa kuzingatia maadili, kujitenga na makundi hatarishi, na kuendeleza juhudi za kujifunza.

Risala ya wahitimu iliyosomwa na Ivetha Emmanuel Kahigi pamoja na kueleza mafanikio ya shule hiyo haikusita kuweka bayana changamoto zake ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nyumba za walimu na vyanzo vya maji vya uhakika.
Longino amewahimiza wazazi na walezi kuzingatia lishe ya wanafunzi kwa kutumia vyema mvua zilizoanza kunyesha.
Mkuu wa shule hiyo mwl Danny Bilabamu akiongea na waandishi wa habari baada ya sherehe ameishukru serikali, wadau na jamii nzima kwa kufanikisha kuanzishwa kwa shule hiyo na kuomba ushirikiano zaidi.

Mahafali hayo yameacha alama ya kipekee katika historia ya shule ya sekondari Runyaga, likiwa ni ishara ya mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio katika sekta ya elimu ikiwa mwanzo wanafunzi wa maeneo hayo walitembea umbali mrefu kufuata elimu katika shule ya sekondari Chakaruru.