Karagwe FM

Mgombea udiwani ACT Wazalendo aahidi zahanati Mabale-Missenyi

5 October 2025, 7:36 pm

Mgombea udiwani kata ya Mabale jimbo la Missenyi mkoani Kagera kupitia chama cha ACT WAZALENDO Sweetbert Kaizilege John. Picha na Theophilida Felician

Kati ya changamoto zilizoko katika kata ya Mabale, Mgombea udiwani ameshtushwa na hali ya kituo kilichojengwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo kutumika kama zahanati ya kijiji cha Kibeo wilaya ya Missenyi mkoani Kagera

Na Theophilida Felician, Bukoba.

Mgombea udiwani kata ya Mabale jimbo la Missenyi mkoani Kagera kupitia ACT WAZALENDO Sweetbert Kaizilege John ameahidi kujenga kituo kipya cha kutolea huduma ya kliniki kwa watoto kitongoji Nyamilembe kijiji cha Kibeo ili kuwanusuru na changamoto wanazokabiliana nazo akina mama na watoto wanaotumia kituo kilichojengwa kwa nguvu ya wananchi kutokana na kituo hicho kuwa katika hali mbaya ya kuchakaa.

Mhandisi Sweetbert ametoa kauli hiyo akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni zake uliofanyika eneo ilipo zahanati hiyo na kusema kuwa hali ya jengo hilo ni hatarishi kwa matumizi kutokana na kuta zake zilizokandikwa kwa udongo kupoteza uimara nakuendelea kubomoka hatimaye kubakia miti pekee.

Mgombea udiwani kata ya Mabale jimbo la Missenyikupitia ACT WAZALENDO Sweetbert Kaizilege John
Mwonekano wa kituo cha kliniki ya mama na mtoto katika kijiji cha Kibeo wilayani Missenyi. Picha na Theophilida Felician

Amesema iwapo atachaguliwa Tarehe 29 Oktoba, 2025 mapema ataanza ujenzi mara moja kabla ya mambo mengine kutokana na uhitaji wa kituo hicho kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi wakimsikiliza mgombea udiwani kata ya Mabale. Picha na Theophilida Felician

Hata hivyo amewahakikishia wananchi kwamba iwapo watampatia nafasi yakuwatumikia atatua changamoto ya maji, barabara na ajira kwa vijana wakata hiyo.