Karagwe FM
Karagwe FM
3 October 2025, 6:41 pm

Mgombea udiwani anayedai kusukumwa na uchakavu wa miundombinu ya soko la Kashai na kwamba anaweza kutatua changamoto hizo kwa kuwa naye ni mhanga.
Na Theophilida Felician, Bukoba
Mgombea udiwani kata ya Kashai manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kupitia chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Bw. Avitus Leopord ameyataja malengo mahususi yaliyomsukuma kugombea nafasi hiyo ikiwemo ya kutatua changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu ya soko la Kashai
Amesema hayo Oktoba 3 mwaka huu wakati wa mahojiano na Radio Karagwe akiwa sokoni humo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa soko bora unahitaji uthubutu wa viongozi na ushirikiano wa wafanyabiashara
Akiongelea vipaumbele atakavyotekeleza ikiwa wananchi watamchagua kwa nafasi ya udiwani bw. Leopold amesema kuwa atahakikisha anashirikiana na wananchi katika marekebisho ya barabara na kuwatetea maafisa usafirishaji juu ya kero zinazowakabili
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara wa samaki katika soko hilo wamekiri kuwepo kwa changamoto na kuwaomba wagombea waliojitokeza kuomba nafasi kuhakikisha wanatatua changamoto hizo
Wamesema kuwa miongoni mwa kero kubwa katika soko hilo ni miundombinu mibovu inayowalazimisha baadhi yao kuhama sokoni hapo