Karagwe FM
Karagwe FM
2 October 2025, 3:15 pm

Wazee katika maeneo mbalimbali nchini wameitumia siku ya wazee duniani kupaza sauti zao kwa serikali wakilalamikia mambo kadha kubwa likitawala suala la huduma duni za afya
Na Theophilida Felician, Bukoba.
Tarehe 1 Oktoba kila mwaka ni siku ya wazee duniani ambapo wazee manispaa ya Bukoba wametumia siku hiyo kwa kutaja changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kero ya ukosefu wa matibabu licha ya serikali kuanzisha mpango wa dirisha la wazee katika vituo vya kutolea huduma ya matibabu hususani hospitali, zahanati na vituo vya afya.
Wakizungumza na Radio Karagwe nyakati tofauti manispaa ya Bukoba mkoani Kagera akiwemo mzee Maulid Rashidi Kambuga wamesema kwamba huduma ya matibabu kwa wazee imekuwa shida hata wanapofika vituo vya kutolea matibabu bado ni changamoto kwao.

Mzee Eliasi Habibu Kateme naye mzee Benadi Mutagwaba Pastory wamefafanua kuwa wazee wamesahaulika katika huduma mbalimbali sababu kuu wakiitaja kutokuwa na jumuia maalumu ya wazee kama yalivyo makundi mengine jambo ambalo lingewasaidia kutatua changamoto zao.

Naye mjumbe wa baraza la wazee mkoa wa Kagera mzee Haruna Idd amesema kwamba hupokea kero nyingi kutoka kwa wazee wenzake wakilalamikia ukosefu wa huduma wanapofika vituo vya kutolea matibabu huku bibi Veronica Rwegi akiiomba serikali kuongeza jitihada katika eneo hilo la matibabu kwa wazee.
Hata hivyo mzee Haruna Iddy Ishengoma ametoa ushauri kwa serikali ukilenga wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu kuhusu namna bora ya kuratibu mipango mahususi itakayowasaidia.
