Karagwe FM
Karagwe FM
19 September 2025, 3:39 pm

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda ameedelea kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kwamba wote wanaofanya uhalifu watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema hayo Septemba 18. 2025 wakati akizungumzia tukio la mauaji ya hivi karibuni katika mji mdogo wa Bunazi wilayani Missenyi yakidaiwa kutekelezwa na mtu ambaye hakujulikana mara moja dhidi ya bi Shadida Shamsi Abdul
Theophilida Feliciani, Bukoba.
Tukio la mauaji ya kikatili dhidi ya Shadida Shamsi Abdul aliyeuawa kwa kuchinjwa shingo nyumbani kwake limeacha simanzi na majonzi makubwa kwa wazazi na wanakijiji cha Nyankele kata ya Mabale wilayani Missenyi anakozaliwa marehemu huyo.
Baba mzazi wa marehemu Shadida mzee Shamsi Abdu akizungumza na redio Karagwe baada ya kufanyika mazishi nyumbani kwake amesema tukio la kuuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo binti yake limewaachia huzuni na simanzi kubwa wao kama familia, ndugu jamaa na wananchi kwa ujumla.

Mzee Abdul ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi CCM kata ya Mabale amesema Shadida mpaka umauti unamkuta alikuwa ni mzazi wa watoto wawili wote wa kiume.
Amewashukuru wananchi waliomfariji wakati wote tangu kutokea kwa msiba huo bila kulisahau jeshi la polisi na madaktari wa kituo cha afya Bunazi, akiliomba jeshi la polisi kufanya jitihada za kuwabaini waliohusika na mauaji ya mtoto wake.

Nao baadhi ya wananchi walioshiriki mazishi ya Shadida wameelezea na namna walivyoshitushwa na uzito wa tukio hilo lenye maumivu makali nao hawakusita kuiomba serikali kudhibiti matukio hayo yakusikitisha.

Hata hivyo watu mbalimbali wametoa salamu za pole akiwemo mgombea udiwani kata ya Mabale kupitia chama cha ACT WAZALENDO Sweetbert Kaizilege John amewaomba familia kuendelea kuwa wamilivu katika kipindi hiki kigumu akiwahakikishia kuwa jeshi la polisi lipo kazini kuwabaini wahusika hoja iliyoungwa mkono na mwenyekiti wa kijiji cha Nyankele.
Hata hivyo kamanda wajeshi la polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda akizungumza na Radio Karagwe kwa njia ya simu amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea tarehe 16, Septemba 2025 katika kitongoji cha Omkitwe mjini Bunazi ambapo mtu mmoja ambaye anasadikiwa kuwa mpenzi wake Shadida alitenda unyama huo kisha kutokomea kusikojulikana na chanzo cha tukio kinadaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.