Karagwe FM
Karagwe FM
29 August 2025, 7:11 pm

Wanaume katika jamii wametakiwa kuripoti ukatili unaofanyika dhidi yao,yakiwemo matukio ya unyanyasaji sambamba na kupigwa na wenza wao majumbani.
Na Theophilida Felician
Shirika la wanaume wanaopitia changamoto kwenye ndoa SHIWACHANDO limeipongeza serikali chini ya wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum kwa kuwatunuku cheti cha utambuzi na pongezi kutokana na majukumu yao ya kupinga ukatili dhidi ya wanaume wanaonyanyasika katika ndoa zao.
Amebainisha hayo mwenyekiti wa shirika hilo na Rais wa wanaume wanaopigwa na wanawake majumbani Ernest Josephat Komba wakati akizungumza na Redio Karagwe kwa njia ya simu kutokea makao makuu ya shirika yaliyopo jijini Dar es Salaam.
Komba amesema shirika la SHIWACHANDO limekuwa likipambana kuwasaidia wananchi hususani wanaume kuyaripoti matukio ya ukatili wanaofanyiwa na wenza wao, matukio ambayo yameendelea kujitokeza katika jamii, hivyo serikali baada ya kuona na kutambua juhudi hizo tayari imewakabidhi cheti kama chachu ya kuongeza bidii ya uwajibikaji .