Karagwe FM

TAMESO (T) yabaini elimu duni kwa waganga wa tiba asili

24 August 2025, 7:00 pm

Katibu mkuu wa chama cha waganga wa tiba asili TAMESO (T) Bw. Lukas Joseph Mlipu. Picha na Theophilida Felician

Chama cha waganga wa tiba asili nchini TAMESO (T) kimebaini changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ushiriki mdogo wa waganga kwenye vikao vya kuwapatia elimu

Na Mwandishi wetu

Chama cha waganga wa tiba asili nchini TAMESO (T) ambacho kimeungana na wadau wengine kupitia wajumbe 15 walioteuliwa na serikali kushiriki zoezi la uhamasishaji wa elimu ya wiki ya tiba asili ya mwafrika kimehitimisha ziara iliyobaini changamoto mbalimbali maeneo yote kilikopitia.

Akizungumza na Radio Karagwe kwa njia ya simu katibu mkuu wa chama hicho ambaye ni miongoni mwa wajumbe hao 15 Bw. Lukas Joseph Mlipu kutokea makao makuu ya chama yaliyopo Kongwa Dodoma baada ya kuhitimisha ziara hiyo wilaya ya Gairo mkoani Morogoro amesema ziara hiyo ilianza mnamo Tarehe 14 Julai na kuhitimishwa Tarehe 23 Agosti 2025.

Amefafanua kuwa ziara nzima amebaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya ushiriki mdogo wa waganga kwenye vikao vya kuwapatia elimu, na maeneo mengi ikiwemo Mwanza, Kagera, Dodoma na Geita waratibu wa serikali kitengo cha baraza la tiba asili na tiba mbadala kutoshiriki vikao hivyo kutoa elimu na baadhi yao kugomea suala la utoaji barua za utambulisho kwa viongozi wa chama kama inavyoelekeza barua ya TAMISEMI.

Katibu mkuu wa chama cha waganga wa tiba asili TAMESO (T) Bw. Lukas Joseph Mlipu

Amendeleea kusema kuwa changamoto hizo zimesababisha mwitikio mdogo wa waganga waliojitokeza kujisajili kushiriki wiki ya tiba asili ya mwafrika hadi sasa wamepata mabanda ya matano kati ya mabanda 21 waliyoyatarajia.

Mbali na hayo amelishukuru jeshi la polisi chini ya mkuu wa polisi nchini (IGP) Camillus Wambura kwa jinsi timu ya wakuu wa polisi mikoa walivyoratibu na kutoa ushirikiano wa hali ya juu kuanzia eneo la usalama hadi kushiriki moja kwa moja kutoa elimu ndani ya vikao jambo lililowatia moyo na nguvu wao kama TAMESOT katika utendaji kazi dhidi ya kuisaidia jamii na serikali eneo hilo la tiba asili.

Mwisho amependekeza elimu ya tiba asili iwe endelevu kupitia vyama na taasisi za serikali badala ya elimu hiyo kutolewa msimu wa wiki ya tiba asili ya mwafrika pekee.