Karagwe FM

Yatima wakabidhiwa nyumba iliyojengwa na Rais Samia Bukoba

24 August 2025, 6:29 pm

Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa (mwenye vazi rangi ya kijani) akiwa na yatima na bibi yao. Picha na Theophilida Felician

Wakati watoto yatima katika maeneo mengi nchini wakitengwa katika makazi ya upweke, hali imekuwa tofauti kwa watoto sita yatima wajukuu wa bibi Catherine Nathanael wa mtaa wa Bulibata kata ya Buhembe manispaa ya Bukoba mkoa wa Kagera.

Na Theophilida Felician, Bukoba, Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa amekabidhi nyumba kwa watoto sita yatima iliyojengwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan baada ya vyombo vya habari kuripoti tukio la nyumba ya bibi yao anayewalea kukumbwa na mafuriko ya mvua.

Nyumba hiyo iliyokabidhiwa kwa watoto hao Tarehe 23 Agost 2025 imejengwa mtaa wa Bulibata kata Buhembe manispaa ya Bukoba.

Hajat Mwassa kabla ya kukabidhi nyumba hiyo amesema kwamba Rais Samia baada ya kuguswa na hali tete ya makazi ya watoto na bibi yao alichukua hatua ya kuwasaidia nyumba ambayo imewekewa miundombinu ya maji, umeme na vyoo vya ndani ili wapate makazi ya kudumu na imara kutokana na makazi ya awali kuathiriwa na mvua iliyosababisha bibi huyo kupoteza vitu vyote vikiwemo vyakula, nguo na magodoro.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Erasto Sima akisoma taarifa kwa mkuu wa mkoa. Picha na Theophilida Felician

Naye mkuu wa wilaya Bukoba Bw. Erasto Sima akitoa taarifa fupi juu ya bibi na changamoto ya makazi yake amesema mnamo Tarehe 10 mwezi Mei. 2024 ilinyesha mvua kubwa iliyosababisha mto kanoni kufurika maji yaliyozingira nyumba za wananchi ikiwemo ya bibi Catherine ambaye alikuwa akiishi mtaa wa Migera kata Nshambya.

Mkuu wa wilaya Bukoba Bw.Erasto Sima
Bibi Catherine Nathanaeli (wa tatu kulia)

Bibi Catherine Nathanaeli akiungana na wajukuu zake hao waliokwisha wapoteza wazazi pande zote amewashukuru wote akiwemo mkuu wa mkoa Fatma Mwassa kwa namna walivyohusika moja kwa moja kutoa misaada mbalimbali kwake tangu kutokea mafuriko hadi anakabidhiwa nyumba na Mhe Rais huku akiwaomba kuendelea kumshika mkono zaidi

Bibi Catherine Nathanaeli
Mwonekano wa nje wa nyumba iliyokabidhiwa