Karagwe FM

Askofu Mndolwa: Chagueni viongozi watakaotekeleza Dira 2050

11 August 2025, 2:44 pm

Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa. Picha na Jovinus Ezekiel

Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera linaadhimisha miaka 40 ya kuanzishwa kwake kwa kukagua na kuzindua miradi mbalimbali iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa

Na Jovinus Ezekiel, Karagwe

Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania Dk Maimbo Mndolwa amewahimiza waumini kuendelea kuliombea taifa wakati huu linapoelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29. 2025 ili taifa lipate viongozi sahihi wa kuwatumikia wananchi.

Askofu mkuu wa kanisa  la Anglikana Tanzania Dkt Mndolwa ametoa wito huo hivi karibuni wakati akihubiri kusanyiko la waumini waliojumuika kwa pamoja katika kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Kagera la Mt. Petro Kayanga wilayani Karagwe mkoani Kagera kwa lengo la kushiriki mwendelezo wa wiki ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 ya kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera ambapo wakati akitoa neno la Mungu kwa waumini hao amewahimiza kuendelea kuombea uchagauzi mkuu na kujitokeza kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba .

Askofu mkuu wa kanisa  la Anglikana Tanzania Dkt Mndolwa
Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa akitoa kipaimara. Picha na Jovinus Ezekiel

Aidha Askofu mkuu Dkt. Mndolwa akiwa kanisani hapo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kanisa la Anglikana Kayanga Dayosisi ya Kagera utakaogharimu zaidi ya shilingi milioni 300 na kutoa  kipaimara kwa wahitimu 36 waliohitimu elimu hiyo baada ya kubatizwa wa kike wakiwa 18 na wa kiume 18 na hapa baadhi yao wanaeleza kuwa elimu hiyo itawafaa kuishi katika misingi ya kumutumikia Mungu.

Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera Darlingtone Bendankeha. Picha na Jovinus Ezekiel

Naye askofu wa kanisa la  Anglikana Dayosisi ya Kagera Darlingtone Bendankeha ameshukuru waumini waliojitokeza kushiriki katika ibada hiyo.

Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa akikagua shughuli za mradi wa shirika la CBIDO. Kushoto ni katibu mtendaji wa CBIDO Mchungaji Flourian Rwangoga. Picha na Jovinus Ezekiel

Hata hivyo ziara ya Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa imehitimishwa kwa kukagua shughuli zinazofanywa na shirika la kuhudumia watu wenye ulemavu wilayani Karagwe CBIDO linalofanya kazi zake chini ya kanisa la Anglikana ambapo ameridhishwa na jinsi shirika hilo linavyowezesha  watoto wenye ulemavu kujifunza stadi za maisha kama ushoanaji,  na  utengenezaji viatu ili waweze kujikimu kimaisha huku akijionea huduma za utengamao kwa watoto wenye ulemavu zinazotolewa katika ukumbi wa Beyond Inclusive (BI) zamani KCBRP mjini Kayanga.