Karagwe FM

‘Ndembo’ watoa wito kuomba amani wakati wa uchaguzi mkuu

27 July 2025, 8:39 pm

Mwenyekiti wa umoja wa wanandembo taifa Omulangi Domina Angribelt Abraham. Picha na Theophilida Felician

Wananchi mkoani Kagera wameendelea kuaswa kutumia nyumba za ibada kuhubiri na kulinda amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu ujao

Na Theophilida Felician Kagera.

Umoja wa wanandembo nchini umeeleza kuungana na watu wengine kuliombea taifa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili uchaguzi huo uweze kufanyika kwa amani na utulivu.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa umoja huo taifa Omulangi Domina Angribelt Abraham akiwa na baadhi ya wanaumoja baada ya kuweka kibao chenye utambulisho wa huduma zao katika mzunguko wa barabara kuu ya Uganda kata ya Rwamishenye manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Mwenyekiti Domina amesema kuwa wao ni watu wanaotoa huduma ya maombezi kwa jamii kupitia ibada za asili kwa sasa wamejikita kuliombea taifa kama ilivyo kwa watu wengine hususan viongozi wa dini na taasisi mbalimbali zenye kuihamasisha amani.

Mwenyekiti wa umoja wa wanandembo taifa Omulangi Domina Angribelt Abraham
Mwenyekiti wa umoja wa wanandembo taifa Omulangi Domina Angribelt Abraham akiwa na baaadhi ya washirika katika umoja wao

Hata hivyo ameongeza kwamba wanafanya hivyo kumuunga mkono Chifu mkuu Hangaya ambaye ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na nia yake njema ya kuunga mkono suala la mila na desturi ambazo zimeanza kupotea kwenye jamii zetu.

Mwenyekiti huyo akiambatana na mwenyekiti wa umoja huo kwa mkoa wa Kagera Donatha Pangarace, baadhi ya waamini wake na balozi wa umoja, pamoja wamesisitiza suala la kuzingatia maadili wakifafanua kwamba kwa sasa kiwango cha maadili kimepungua kwenye jamii makundi yote watoto kwa wakubwa hali siyo nzuri.

Balozi wa wanandembo Richard Leonard Mushashu amebainisha kuwa kushuka kwa maadili kumechangia baadhi ya matukio maovu ya wizi, ulevi, mauaji na mifarakano katika familia ambapo amesisitiza jamii iludi kwenye mstari na kuzingatia mila na desturi zinazosaidia kuijenga jamii iliyo bora.