Karagwe FM

Kagera yawezeshwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko

16 July 2025, 8:20 pm

Mkurugenzi wa dharura na maafa wizara ya afya Dkt Erasto Sylvanus (wa kwanza kushoto) akikabidhi vifaa kwa katibu tawala wa mkoa wa Kagera Stefano Mashauri Ndaki. Picha na Theophilida Felician

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeikabidhi serikali ya Tanzania msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 112 kwa ajili ya kurejesha hali ya awali ya huduma za kiafya katika maeneo yaliyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg.

Na Theophilida Felician

Mkoa wa Kagera umetakiwa kujipanga vizuri kwa kujiweka tayari kuzuia na kudhibiti magonjwa ya mlipuko.

Ametoa wito huo mkurugenzi wa dharura na maafa wizara ya afya Dr Erasto Sylvanus wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa tiba mkoa wa Kagera vilivyotolewa na shirika la afya duniani WHO chini ya mwakilishi mkazi wa shirika hilo Dr Galbert Fedjo shughuli iliyofanyika viunga vya ofisi ya mkuu wa mkoa manispaa ya Bukoba.

Dr Erasto amesema Kagera ni miongoni mwamikoa inayopakana na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda hivyo mwingiliano wa jamii ni mkubwa jambo ambalo bila kuchukua tahadhari upo uwezekano wa kueneza magonjwa.

Mkurugenzi wa dharura na maafa wizara ya afya Dkt Erasto Sylvanus

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda 20 na magodoro yake, ndoo 86, mashine 5 za kufulia nguo na Cardiac monitors 20.

Hata hivyo amewashukuru WHO kwa msaada huo wenye kulenga na kuongeza nguvu juhudi za serikali katika kuimarisha afya za jamii.