Karagwe FM

John Mrema: Kagera puuzeni wanaopinga uchaguzi

15 July 2025, 7:23 pm

Mkurugenzi wa mawasiliano na taarifa kwa umma wa chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) John Mrema (upande wa kulia). Picha na Theophilida Felician

Chama cha Ukombozi wa Umma kimeanza ziara yake Kanda ya Viktoria kufuatilia idadi ya watia nia ya ubunge kwa ajili ya uchaguzi mkuu 2025

Na Theophilida Felician, Bukoba

Chama cha ukombozi wa umma CHAUMMA kimetoa wito kwa wananchi mkoani Kagera kuzipuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa zikiwahamasisha kutoshiriki uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano na taarifa kwa umma wa chama hicho John Mrema akiwa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera akisema kuwa mtu kuwahimiza wananchi kutoshiriki uchaguzi ni kuwanyima haki yao ya kikatiba hivyo watu wa namna hiyo ni wa kupuuzwa kwa namna yoyote ile kwani jambo hilo ni la hatari.

Mkurugenzi wa mawasiliano na taarifa kwa umma wa chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) John Mrema

Katika ziara hiyo iliyolenga kupokea taarifa ya watia nia ya kugombea ubunge na udiwani imevuna wanachama wapya wa CHAUMMA kutoka chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Muleba kaskazini kutoka kata nane wakiongozwa na katibu wa jimbo Esta Rweyongeza.

Hata hivyo watia nia kadhaa kupitia CHAUMMA wametangaza kuwania nafasi za udiwani na ubunge majimbo ya Kagera na Geita.

Amewasihi wananchi kukiunga mkono CHAUMMA ili kiweze kuleta mageuzi ya hali ya juu kama ilivyo kiu ya wananchi.

Esther Fulano ni naibu Mkurugenzi sheria, katiba na haki za binadamu kanda ya Victoria ameeleza tayari ipo mikakati madhubuti itakayosaidia kuwapata wagombea wazuri watakaoyapambania mabadiliko ya kweli hasa hasa kanuni na sheria za uchaguzi huku akisisitiza kuwa CHAUMMA imeandaa mikakati imara itakayosaidia kuidhibiti CCM kutovitumia vyombo vya dola kwenye uchaguzi

Naibu mkurugenzi wa sheria, katiba na haki za binadamu kanda ya Victoria Esther Fulano